Mtandao mpya unaoundwa na
Radio na vyombo vya habari vya kijamii Tanzania chini ya shirika la
vyombo vya habari vya maudhui ya kijamii uliosajiliwa kwa jina la
TANZANIA DEVELOPMENT INFORMATION ORGANIZATION-TADIO umeanzishwa rasmi
baada ya kuvunjika kwa mtandao wa zamani wa COMNETA.
Tukio hilo limetokea Julai 28,
2017 katika mkutano mkuu wa kwanza ambao pamoja na mambo mengine
ulichagua safu mpya ya viongozi wa mtandao huo. Shirika la mtandao wa
vyombo vya habari jamii Tanzania uliokuwa na jina la COMMUNITY MEDIA
NETWORK OF TANZANIA – COMNETA, limevunjika rasmi mwezi machi mwaka huu.
Katika mkutano huo kuwa kuundwa
kwa shirika hilo jipya kunalenga kuhakikisha kunakuwa na mtandao makini
wa Radio na vyombo vingine vilivyojikita katika kuibua kwa kuandika na
kutangaza masuala ya kijamii kwa ajili ya maendeleo.
Akihutubia katika mkutano huu
kaimu mkuu wa ofisi ya UNESCO Tanzania, ambao ni wafadhili wakubwa wa
mtandao huo Bw. Christophe Legay kwa niaba ya Mkuu wa ofisi Bi. Zulmira
Rodrigues amepongeza hatua iliyofikiwa na Radio wanachama ya kuunda
mtandao mpya.
Alieleza kuwa UNESCO itaendelea
kufanya kazi bega kwa bega na shirika hilo jipya la TADIO ili
kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata huduma sahihi za kihabari
zitakazosaidia kuboresha maisha yao na kuchochea maendeleo ya upashanaji
wa habari nchini.
Bw. Christophe amehimiza kwamba
vyombo vya jamii vinao wajibu mkubwa wa kuhakikisha sauti za watu
wanaowahudumia hasa wanaoishi vijijini.
Aliwaasa kushughulika na masuala ya kibinadamu na si watu binafsi.
Wakati huo huo Mtandao huo
unaoundwa na jumla ya Radio 32 kutoka katika mikoa mbalimbali ya
Tanzania bara na Zanzibar, umefanya uchaguzi mkuu na kuwapata viongozi
watakaosimamia shughuli zake kwa miaka mitatu ijayo.
Uchaguzi huo ulitanguliwa na tukio
la kujiuzuru kwa viongozi wa mpito waliochaguliwa mwezi Machi mwaka
huu, baada ya kutangazwa rasmi kuvunjika kwa muungano wa awali wa radio
jamii wa COMNETA.
Akitangaza matokeo, msimamizi wa
uchaguzi huo ambae pia ni mlezi wa ushirika huo, Balozi mstaafu
Mheshimiwa Christopher Liundi, alimtangaza Bw. Prosper Kwigize aliyekuwa
mgombea pekee kuwa Mwenyekiti mpya baada ya kupata kura za ndiyo 26
kati ya kura 30 zilizopigwa na wajumbe waliohudhuria.
Balozi Liundi, pia alimtangaza Bw.
Marco Mipawa kuwa Katibu Mtendaji baada ya kupata kura 28 za ndiyo,
Aidha Mipawa pia alikuwa mgombea pekee katika uchaguzi huo.
Viongozi wengine waliochaguliwa ni
pamoja na Mweka Hezina, Shaaban Ali Makame aliepata kura 24 za ndiyo.
Pia mkutano huo uliwachagua wajumbe sita wa Bodi ya shirika hilo la
TADIO ambao ni Maimuna Msangi kutoka Pangani FM, Gladys Mapeka kutoka
Radio Kilosa, Ali Mbarouk Omar kutoka kutoka Klabu ya Waandishi wa
Habari wa Pemba (PPC), Ali Khamis kutoka Adhana FM Zanzibar, John
Baptist kutoka Dodoma FM na Anthony Masai kutoka Triple A FM.
Akizungumza baada ya kutangaza
matokea hayo, Balozi Liundi aliitaka safu ya uongozi mpya kuongoza kwa
kufuata katiba na malengo ya shirika hilo kwa lengo la kutetea maslahi
mapana ya wananchi kwa kupitia kazi zinazofanywa na radio za kijamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya
wa TADIO Bw. Prosper Kwigize amewashukuru wajumbe kwa kuchagua safu mpya
ya uongozi na kuahidi kujenga ushirikiano mpya ambao utawezesha
kufikiwa kwa malengo ya kuanzishwa kwa mtandao huo wa ushirikiano wa
vyombo vya habari vya kijamii.
Bw. Kwigize ametoa wito kwa wadau
wengine hususani Radio za kitaifa, magazeti, waandishi wa habari za
mitandaoni (bloggers) Muungano wa wamiliki wa vyombo vya habari MOAT,
TAMWA, MISA, Baraza la Habari Tanzania, Runinga na Vilabu vya waandishi
wa habari mikoani kushirikiana na shirika la TADIO ili kutoa huduma
stahiki kwa jamii.
Amehimiza pia serikali na taasisi
zake kutoa ushirikiano kwa TADIO ili misimamo, dira na malengo
yanayoibuliwa na serikali yawafikie wananchi kwa haraka kupitia muungano
huo wa Radio za mikoani.
Amesisitiza kuwa, mtandao huo wa
TADIO una ofisi na studio ya kisasa ndani ya Chuo Kikuu Huria Tanzania –
OUT makao makuu Kinondoni Dar es Salaam ambako kazi ya ofisi na studio
hiyo ni kuratibu shughuli za mtandao pamoja na kuandaa vipindi ambavyo
vitakuwa vikisambazwa kwa radio wanachama.
Aliitaka safu ya uongozi mpya
kuacha kufanya kazi kwa mazoea, kujenga umoja na mshikamano pamoja na
kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili kuyafikia malengo ya ushirika huo.
Mtandao wa TADIO unafadhiliwa na UNESCO chini ya mradi wa SIDA/SDC.
No comments:
Post a Comment