Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa akisoma Hotuba ya Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha
Wauguzi Tanzania (TANNA) ambao umeanza leo Oktoba 4,2017 Mkoani Lindi
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
akisalimiana na Katibu Mwenezi msaidizi wa Chama cha Wauguzi Tanzania
(TANNA) Johari Yusuf, baada ya ufunguzi wa Mkutano wa chama cha wauguzi
leo Oktoba 4,2017 Mkoani Lindi.katikati ni mweye beji shigoni ni Rais
wa Chama cha Wauguzi Tanzania Bwana Poul Magesa .kulia kwa katibu
mwenezi ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wauguzi Tanzania Sebastian Luziga.
PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
……………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amepiga marufuku tabia ya baadhi ya viongozi katika maeneo mbalimbali
nchini kuwakamata na kuwaweka ndani watumishi wakiwemo wauguzi bila ya
kufuata taratibu.
Pia amewataka wauguzi nchini
kufanya kazi kwa weledi, uaminifu pamoja na kufuata maadili ya taaluma
yao kwa kuwa maisha ya wagonjwa yako chini yao.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo
(Jumatano, Oktoba 04, 2017) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa 45
wa Chama cha Wauguzi Tanzania, mkoani Lindi.
“Naagiza viongozi wote kufuata na
kuzingatia sheria. Kama kuna makosa ya kitaaluma, Mabaraza husika
yashughulikie jambo hilo na ni marufuku kuwaweka ndani watumishi kwa
tuhuma za kitaaluma.”
Amesema kwamba katika sekta ya
afya bila wauguzi ambao ni kundi kubwa kati ya Wanataaluma wa Afya,
Serikali haitaweza kutekeleza ipasavyo mikakati mbalimbali iliyopangwa
kwa ajili ya kuboresha sekta hiyo.
Katia hatua nyingine Waziri Mkuu
amewaasa wauguzi wote nchini kuhakikisha wanazingatia kiapo cha maadili
ya kazi yao na kwamba Serikali haitamvumilia yeyote atakae bainika
kwenda kinyume.
“Nanyi Wauguzi mnao wajibu wa
kutoa huduma kwa wananchi kwa kuzingatia kiapo na miiko ya taaluma yenu.
Tunazo taarifa kuhusu baadhi ya Wauguzi kutoa lugha chafu kwa wagonjwa,
kuomba rushwa na wengine kujihusisha na vitendo vya wizi wa dawa.”
Amesema lengo la Serikali ni
kuhakikisha afya za Watanzania wote zinaimarika ili kuendana na kasi ya
utendaji kazi wa Serikali ya kuinua uchumi na kufikia wa kiwango cha
kati, hivyo ni lazima watoe huduma bora kwa wananchi.
Pia amewaomba waunge mkono kwa
nguvu zote jitihada za Serikali katika kuhakikisha miundombinu na vifaa
vyote havihujumiwi na watu wachache ili viwe msaada mkubwa hususani kwa
akina mama wajawazito ili wajifungue salama.
Akizungumzia kuhusu upungufu wa
wauguzi nchini, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuajiri
watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo Wauguzi na Wakunga na kuwapanga
katika maeneo yenye upungufu zaidi.
Awali, Naibu Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Khamis Kigwangalla
alisema baadhi ya viongozi katika maeneo mbalimbali wamekuwa
wakiwakamata na kuwachukulia hatua watumishi wa Sekta ya Afya bila ya
kufuata taratibu, jambo ambalo si sahihi.
Mkutano huo umehudhuriwa Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Kigwangalla, Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania Bw. Paul Magesa, Mbunge
wa Lindi Mjini Bw. Hassan Kaunje, Mbunge wa Kuteuliwa Mama Salma
Kikwete(MB) Viti maalum.
Wengine ni Mkurugenzi wa Huduma za
Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Bw. Gustav Moyo, Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga
Tanzania Bw. Stewart Mbelwa.
Wengine ni Mbunge wa Viti Maalumu,
Hamida Abdallah, Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo ya Uuguzi Bw.
Ndementria Vermund, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania Dkt. Obadia
Nyongole na wawakilishi wa wauguzi kutoka mikoa yote nchini.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, OKTOBA 04, 2017.
No comments:
Post a Comment