MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu
imeahirisha kesi ya utakatishaji fedha na kugushi inayowakabili Rais wa
Simba, Evans Aveva na Makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ hadi October
11, 2017 kwa sababu upelelezi haujakamilika.
Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU,
Leornad Swai amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa kuwa shauri
hilo limeitishwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilika, hivyo
anaomba ipangiwe tarehe nyingine ambapo baada ya kueleza hayo Hakimu
Mwambapa aliahirisha kesi hiyo hadi October 11, 2017.
Evans Aveva na Makamu wake,
Geofrey wanakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka
ya uongo na kutakatisha Dola za kimarekani 300,000.
Katika shtaka la kwanza,
washtakiwa hao wanadaiwa kuwa walikula njama ya kughushi fomu ya maombi
ya kuhamisha fedha ya March 15, 2016 wakionesha Klabu ya Simba inalipa
mkopo wa Dola za kimarekani 300,000 kwa Evans Aveva wakati si kweli.
Katika shtaka la pili alidai
kuwa March 15, 2016 katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe Ilala, Aveva
akijua alitoa nyaraka ya uongo ambayo ni fomu ya maombi ya kuhamisha
fedha ya March 15, 2016 wakati akijua ni kosa.
Katika la tatu la kutakatisha
fedha, Aveva na Nyange wanadaiwa kuwa kati ya March 15 na June 29, 2016
Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha fedha kwa kupata
Dola za kimarekani 300,000 wakati wakijua ni zao la uhalifu.
Kwa upande wa shtaka la nne la
kutakatisha fedha, Aveva anadaiwa kuwa kati ya March 15, 2016 katika
benki ya Barclays Mikocheni alijipatia Dola za kimarekani 300,000 wakati
akijua zimetokana na kughushi.
Katika shtaka la tano la
kutakatisha fedha, mshtakiwa Nyange anadaiwa kuwa March 15, 2016 katika
benki ya Barclays tawi la Mikocheni alimsaidia Aveva kujipatia Dola za
kimarekani 300,000 wakati akijua fedha hizo zimetokana na kughushi.
Washtakiwa wapo rumande kwa sababu shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili halina dhamana.
No comments:
Post a Comment