Jamii ya wazanzibari imeshauriwa
kufikiria mikakati na huduma bora zitakazosaidia kupunguza idadi ya
kuzaliwa na kufariki watoto njiti ili ambao wanakuwa mzigo kwao na
Serikali kwa jumla.
Ushauri huo umetolewa na Katibu
Mkuu Wizara ya Afya Bi. Asha Ali Abdalla alipokuwa akitoa tamko kwa
waandishi wa habari kuhusu siku ya maadhimisho ya watoto njiti duniani
katika ukumbi wa Wizara hiyo Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Alisema sababu ya kufanyika
maadhimisho ya watoto njiti duniani sio kuwabeza watoto hao lakini ni
kuamsha hisia na kuinua uwelewa kwa wananchi na watoa huduma ya afya ya
watoto hao kwani iwapo hatua zinazofaa hazitachukuliwa wataendelea
kuzaliwa na kufariki kwa idadi kubwa.
Alisisitiza kuwa Shirika la Afya
duniani linaamini kuwa vifo vya watoto njiti vinaweza kuepukika kwa
silimia 75 iwapo jamii ikishirikiana na Serikali wataweka mkazo huduma
za kinga, ugunduzi wa matatizo mapema na matibabu bora na kwa wakati
stahili.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya
alikumbusha kuwa takriban watoto wote wanaozaliwa njiti wanakuwa na
matatizo mengi ya kiafya yanayohitaji huduma za haraka kwa uokozi wa
maisha yao.
Alisema huduma hizo mara nyingi
zinakuwa mzigo usiotarajiwa kwa familia, ndugu na jamaa na kupelekea
changamoto nyingi zikiwemo za uzalishaji kiuchumi.
Alitanabahisha kuwa suala la
msingi ni kufanyakazi kwa pamoja katika kutoa huduma sahihi na rahisi
zitakazopelekea kupungua kuzaliwa watoto njiti vyenginevyo Zanzibar
haitaweza kufikia lengo kuu la kumaliza vifo vinavyoweza kuepukika kwa
watoto wachanga ifikapo mwaka 2030.
Alisema Wizara ya Afya imejipanga
kutoa elimu ya Afya juu ya matatizo yanayochangia kuzaliwa watoto njiti,
kuimarisha huduma zao katika ngazi zote na kuongeza wataalamu wanaotoa
huduma za watoto njiti katika ngazi za hospitali, vituo vya afya na
katika jamii.
Akieleza ukubwa wa tatizo la
watoto njiti Katibu Mkuu alieleza kuwa takwimu kutoaka hospitali ya
Mnazimmoja pekee zinaonesha kuwa kati ya watoto 347 waliofariki watoto
njiti walikuwa 154 ambao ni asilimia 44.
Alizitaja sababu za kuzaliwa
watoto njiti ni pamoja na maradhi yasiyoambukiza, wajawazito wenye umri
chini ya miaka 20 na zaidi ya mika 40, kuwa na maambukizi wakati wa
ujauzito, utumiaji wa dawa za kienyeji wakati wa ujauzito na ulemavu
katika viungo vya uzazi.
Watoto njiti ni kizazi hai ambacho
huzaliwa kabla ya kutimia wiki 37 za ujauzito ambapo kilele cha
maadhimisho hayo hufanyika kila ifikapo tarehe 17 Novemba na kauli
mbiu ya mwaka huu TUFANYE KAZI KWA PAMOJA KUWATUNZA WATOTO
NJITI.
Wakati huohuo Muuguzi Mkuu wa
hospitali ya Mkoa wa kaskazini Unguja Mwanamvua Said alisema kuwa ulezi
wa watoto njiti unahitaji ushirikiano mkubwa kati ya hospitali na wazazi
ili kudumisha afya ya watoto hao.
Muuguzi huyo alitoa ushauri huo wakati wa maadhimisho ya mtoto njiti yaliyofanyika kimkoa katika hospitali ya Kivunge.
Aliwataka wazazi kuacha tabia ya
kuwalaza watoto njiti kwenye magodoro kwani kufanya hivyo kunaweza
kuathiri afya ya mtoto kutokana na joto kali la magodoro.
No comments:
Post a Comment