HATIMAYE Menejimenti ya Kampuni ya TanzaniteOne iliyoko Mirerani wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara, imemvua madaraka Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa mgodi wa madini ya tanzanite, Manu Sharma kwa tuhuma za kuwanyanyasa wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Mbali ya kuvuliwa nafasi hiyo, pia uongozi umemng’oa katika nafasi ya Uhasibu Mkuu na Idara ya Manunuzi zilizokuwa zikishikiliwa na Sharma kwa muda mrefu kutokana na malalamiko ya wafanyakazi kuwa wanacheleweshewa mishahara na kushindwa kulipa malipo mbalimbali kwa wakati, hali iliyofanya ufanisi wa kazi kuwa chini.
Kuondolewa katika nafasi hiyo, kumethibitishwa na Sharma alipozungumza na gazeti hili kwa simu, akisema hana kinyongo kwa maamuzi yaliyochukuliwa, lakini alikataa kusema hatima yake baada ya maamuzi hayo ya menejimenti.
“Ni kweli nimevuliwa madaraka, lakini sina cha kusema zaidi ya hilo ila niko bado kazini,” alisema Sharma, ambapo sasa Menejimenti ya TanzaniteOne imemteua raia wa Uingereza, Robert Grafen Greaney maarufu kwa jina la Robert GG kuwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mgodi huo.
Greaney pia amekabidhiwa Kitengo cha Manunuzi, ambacho kilikuwa kikilalamikiwa kwa kununua zana za uchimbaji zisizo na kiwango na chakula kibovu kwa wafanyakazi.
Uongozi wa Kampuni ya TanzaniteOne katika vikao vyake vya siku tatu mfululizo ndani ya mgodi huo, umemteua Saitoti Saibul kuwa Mhasibu Mkuu wa Kampuni hiyo na Sharma sasa amekabidhiwa Kitengo cha Teknolojia ya Mawasiliano (IT).
Sharma alikuwa akituhumiwa kunyanyasa wafanyakazi kwa ubaguzi wa rangi dhidi ya Waafrika hususan Watanzania, wanaofanya kazi TanzaniteOne na kuwalisha vyakula vya pilipili ni moja ya sababu kubwa iliyofanya uongozi kuchukizwa na kuamua kuchukua hatua za haraka dhidi ya mhusika, kwani malalamiko ya wafanyakazi ni sahihi.
Wiki iliyopita gazeti hili liliripoti malalamiko ya wafanyakazi wa TanzaniteOne, ambao waliomba kutotajwa majina, wakidai kuwa chakula wanachokula hakistahili kuliwa kwani ni kibovu na kinawekwa pilipili nyingi. Aidha, walimtuhumu kwa kuchelewesha mishahara yao bila sababu za msingi.
“Wafanyakazi wanadai stahili zao kama vile mishahara na posho ya masaa ya ziada, lakini Sharma halipi anakalia malipo akiulizwa hana jibu na hufika mahali huwatukana Watanzania kwa kudai haki yao, lakini wale wa kigeni wanalipwa haraka, huu si ubaguzi mkubwa,” mfanyakazi mmoja aliliambia gazeti hili wiki iliyopita.
No comments:
Post a Comment