RAIS John Magufuli ameiagiza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuharakisha mchakato wa kutayarisha Sera ya Diaspora, itakayotumika kama mwongozo wa kushirikisha jamii ya Watanzania waishio nje ya nchi kuchangia kukuza uchumi.
Alisema hayo kupitia hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, wakati akifunga mkutano wa Diaspora mjini Unguja jana.
Alisema kuwepo kwa Sera ya Diaspora kutaifanya jamii hiyo kushiriki kuchangia maendeleo ya taifa katika uwekezaji, hivyo kuinua uchumi.
Alisema malengo ya Serikali ni kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 katika sekta ya viwanda, uwekezaji, kilimo na utalii ili kukuza pato la Taifa.
“Naiagiza Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuharakisha mchakato wa kutayarisha Sera ya Diaspora ambayo itatoa nafasi kwa jamii kushiriki kuchangia kukuza uchumi na kuzalisha ajira kutokana na uwekezaji wao,” alisema Rais Magufuli.
Aliwaambia wana Diaspora kwamba Serikali ipo kwenye mikakati ya kukuza uchumi na sekta ya uwekezaji pamoja na uwajibikaji na kupambana na rushwa sehemu ya kazi.
“Nimedhamiria kukusanya kodi, kupunguza rushwa, kupambana na ufisadi katika sehemu za kazi na uwajibikaji, ili kuweka nidhamu inayotakiwa serikalini,” alisema.
Akizungumzia uraia pacha, alisema ni muhimu kwa ajili ya mustakabali wa maendeleo kwa Watanzania waliopo ughaibuni.
Alisema serikali imejizatiti kulishughulikia hilo kikamilifu kwa ajili ya kuona mchango wa Diaspora unainufaisha Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine ziliopo katika Bara la Afrika
No comments:
Post a Comment