TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), imetakiwa kuhakikisha tafiti inazozifanya zinatoa matokeo yatakayoweza kutatua matatizo ya wananchi, kuendelea kutengeneza ajira ili kuinua kipato cha wananchi na uchumi wa taifa.
Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, wakati akifungua Kongamano la Tano la kitaifa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu. Alisema tafiti hizo zilenge kuimarisha uchumi wa viwanda.
Alitaka watambue kuwa mchango wao ni muhimu katika kuinua uchumi. Pia aliwataka watafiti kuhakikisha matokeo ya tafiti wanazozifanya yanawafikia walengwa ili wayatumie kukuza uzalishaji na utoaji huduma za maendeleo.
“Watu wamekuwa wakisema matokeo ya tafiti mnazozifanya hayawafikii hivyo kufanya hivyo bila kuhakikisha zinawafikia, hatutafaidika na tafiti mnazozifanya. Toeni matokeo kwa walengwa kadiri mnavyofanya tafiti zenu,” alisema.
Alisema kwa kuthamini shughuli zinazofanywa na tume hiyo, serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017 imetenga Sh bilioni 12.8 kwa ajili ya kuwekeza kwenye utafiti, hivyo ameiagiza tume hiyo kuhakikisha inatumia vizuri fedha hizo ili kuleta matokeo yanayotarajiwa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.
“Serikali inalenga uchumi wa viwanda, hivyo itaendelea kuimarisha matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu, kwa lengo la kuchagiza ukuaji wa viwanda na ushindani,” aliongeza na kuishukuru Serikali ya Afrika Kusini kwa kukubali kushirikiana na Tanzania kwenye masuala ya utafiti.
Kwa upande wake, Balozi wa Afrika Kusini nchini, Thami Mseleku, aliipongeza tume hiyo kwa kazi nzuri.
Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk Hassan Mshinda, alisema watafiti wamepata fursa ya kuwasilisha matokeo ya miradi 15 iliyofadhiliwa na Serikali, pamoja na Serikali ya Afrika Kusini tangu mwaka 2013. Kila nchi ilichangia zaidi ya Sh milioni 500
No comments:
Post a Comment