Serikali Yatoa Siku 14 kutatua changamoto za watumishi Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI)
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ametoa siku 14 kwa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Mifupa (MOI) kuangalia matatizo yaliyopo na kuyafanyia tathmini, huku akisisitiza kambi za upasuaji zirejee na zianze kazi mara moja ifikapo Agosti 13, mwaka huu.
Alisema bodi hiyo itakapokaa na kurudisha majibu kwake atafanya maamuzi likiwamo suala la uteuzi wa mkurugenzi wa taasisi hiyo, akisema imekaimiwa kwa kipindi kirefu na sasa ni wakati wa kumpata wa kuishikilia.
“Kitu kinachonisumbua kichwa kwa sasa ni kuhusiana na kambi za upasuaji, naomba zianze kazi mara moja, wanaoteseka ni wananchi wa hali ya chini maana baada ya kufutwa kambi za upasuaji ikaanzishwa kambi ya upasuaji wa watu wanaolipia, wasiojiweza wanahudumiwa vipi?” alihoji.
Kauli ya Ummy imekuja baada ya kikao cha ndani alichokifanya jana na wafanyakazi wa taasisi hiyo, ambao walitoa malalamiko mbalimbali kuhusu utendaji wa taasisi, stahiki zao pamoja na malalamiko mengine waliyoyaandika kwenye makaratasi na kuwasilisha kwake.
“Baada ya kuwaambia muandike kwenye vikaratasi, nimegundua kwamba mlishindwa kusema wazi ila molari ya wafanyakazi ipo chini na baada ya kusoma kwa makini nimegundua hakuna ushirikiano wa kutosha,” alisema Ummy.
Ummy alisema katika kutatua changamoto kadhaa ndani ya taasisi ataanza kwa kupeleka CT Scan mpya, lakini pia bajeti ya vifaa tiba kiasi cha Sh3 bilioni.
Aliunga mkono wazo la madaktari wa taasisi hiyo ambao walimtaka kupeleka muswada bungeni wa kupitisha sheria ya malipo ya kuchangia huduma katika mfuko wa Trauma Fund kwa watu wote wanaotumia vyombo vya usafiri ili kuokoa maisha ya wagonjwa wanaopata ajali.
“Naunga mkono hoja hii, lakini siwezi kuisemea moja kwa moja mpaka ipate baraka kutoka Baraza la Mawaziri, maana ninachokitaka ni kusaidia maskini wasiojiweza ambao ndiyo hao kila siku wanagongwa na pikipiki na magari, ndiyo wahanga wa hizi ajali,” alisema Ummy.
Akizungumza kwa msisitizo, Ummy alisema lengo lake kubwa ni kuhakikisha sekta ya afya inakuwa bora kwa kipindi chake atakachokuwa waziri wa afya huku akiahidi kushughulikia kero mbalimbali za wafanyakazi walizoziwasilisha kwake.
Akizungumza awali Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Mifupa (MOI) Dk Othman Kiloloma alisema wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo motisha na posho kwa wafanyakazi.
Alisema deni la MOI limekuwa sababu ya Taasisi kukosa vifaa na vitendanishi kwa wakati kutokana na wasambazaji wengi kushindwa kuhudumia.
Dk Kiloloma alisema mwaka 2014 wakati anapokea Taasisi hiyo kama Kaimu Mkurugenzi alikutana na deni kubwa la stahiki za wafanyakazi kiasi cha Sh4 bilioni pamoja na deni upande wa Saccos kiasi cha Sh500 milioni na kwa sasa wamefanikiwa kulipia Sh600 milioni.
Alisema jengo jipya la MOI bado linahitaji kiasi cha Sh20.6 bilioni ili kukamilisha vifaa vinavyohitajika ikiwemo samani muhimu.
“Tatizo kubwa tunalopambana nalo hivi sasa ni jengo jipya la MOI, ambalo bado hatujakabidhiwa mpaka sasa, kwanza lina upungufu mkubwa ikiwemo lifti kutokufanya kazi, jengo zima ili likamilike linahitaji kiasi cha Sh8.6 bilioni,”alisema Dk Kiloloma.
Wafanyakazi wafunguka
Wakitoa malalamiko yao kwa Waziri, wafanyakazi hao walizungumzia mambo makubwa manne likiwemo la stahiki ya mishahara yao na malipo, uchakavu wa vifaa tiba, maendeleo ya rasilimali watu na mrundikano wa wagonjwa.
Pamoja na mambo mengine wafanyakazi hao walilalamikia suala la kutopandishwa vyeo, kutopanda kwa mishahara na malipo ya ziada kuwa hayatoshelezi, huku wengine wakifanya kazi kwa miezi sita bila malipo.
Mmoja wa wauguzi wa MOI, Mwajabu Ali alisema vitanda vilivyopelekwa na Rais John Magufuli baada ya kuzuiwa kwa mchapalo, vimekuwa na upungufu mkubwa ikiwemo kukosa matairi, jambo ambalo linaleta ugumu wa utoaji wa huduma.
Alisema jengo hilo jipya limekuwa na matatizo ya lifti, hivyo inakuwa kazi kubwa kumsafirisha mgonjwa kutoka wodini mpaka kumfikisha katika chumba cha upasuaji au kipimo.
“Tunafanya kazi katika mazingira magumu, vitanda havina matairi, lifti mbovu, hakuna maji, oksijeni za ukutani hakuna, tunatumia mitungi ambayo hata hivyo ni mizito sana kuibeba,”alisema Mwajuma.
Mtaalamu wa usingizi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi MOI, Lucas Magwisa alisema wauguzi wanafanya kazi katika mazingira magumu kutokana na stahiki zao kuwa tofauti na madaktari ambao hata hivyo kazi nyingi wanazifanya wao.
Kaimu Mkurugenizi wa MOI Dkt. Othman Kiloloma akizungumza mbele ya watumishi wa Taasisi ya mifupa muhimbili (MOI) hawapo pichani kabla ya kumkaribisha Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu hayupo pichani wakati alipokwenda kusikiliza changamoto za watumishi hao jijini Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment