WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Tanzania iko tayari kujifunza kutoka kwa nchi wanachama wa Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora barani Afrika (APRM) ili iweze kuboresha hatua ilizofikia kwenye mpango huo.
Alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati akichangia mada katika Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora barani Afrika (APRM Forum) uliofanyika kwenye Hoteli ya InterContinental jijini Nairobi, Kenya.
“Nitumie fursa hii kukitaarifu kikao chako kwamba Tanzania imeshaanza kutekeleza mpango kazi wa kitaifa uliojikita kutatua changamoto katika sekta za maji, elimu, kilimo, nishati na miundombinu kama zilivyoainishwa kwenye kikao cha APRM,” alisema.
Tanzania ilifanyiwa tathmini Januari, 2013 kwenye kikao cha Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika kilichofanyika Addis Ababa, Ethiopia. Mapema, akifungua mkutano huo, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alisema viongozi wa Afrika hawana budi kukubaliana na kuungana kutafuta suluhisho katika ushindani wa kibiashara.
Alisema nchi wanachama wa mpango huo wanapaswa kujenga umoja kama njia muafaka ya kufikia makubaliano hayo. Wakati huohuo, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, alisema Bara la Afrika linakabiliwa na changamoto 11 zinazokwamisha maendeleo na kutaka zitafutiwe ufumbuzi ili kuzisaidia nchi nyingi barani humo.
Akiwasilisha mada binafsi katika mkutano huo, Rais Museveni alisema kwa zaidi ya miaka 50, amekuwa kiongozi katika sehemu kadhaa na kwamba amebaini kuwa changamoto hizo zimezuia ukuaji wa uchumi barani humo, pamoja na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.
Alisema asilimia kubwa ya changamoto hizo haikupata ufumbuzi hata wakati Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) yalipokuwa yanatekelezwa.
Alitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni mikanganyiko ya kiitikadi ambayo huzaa ubinafsi na maslahi binafsi, kuwepo kwa mataifa dhaifu, nguvu kazi duni (kitaaluma na kiafya), uduni wa miundombinu (barabara, maji, umeme, tehama) ambao unashindwa kuvutia uwekezaji, uhaba wa viwanda unaolazimisha nchi kusafirisha mali ghafi na uhaba wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa barani Afrika
No comments:
Post a Comment