• Breaking News

    ..

    ..

    Sunday, 28 August 2016

    Viongozi tatueni kero za polisi



    WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amewaagiza viongozi wa Jeshi la Polisi na wakuu wa vitengo ndani ya jeshi hilo, kuhakikisha wanatatua kero mbalimbali zinazowakabili askari kutokana na kazi kubwa wanayoifanya ya kulinda usalama wa raia na mali zao.
    Aidha amesema kuwa ametembelea makazi ya askari na kugundua kuwa kuna haja ya kujenga nyumba za kisasa kwa ajili yao na kuwaondolea kero ya makazi kutokana na nyumba wanazoishi kwa sasa kutokidhi mahitaji ya familia zao.
    Waziri Mwigulu aliyasema hayo jana jijini hapa wakati akizungumza na wakuu wa vitengo kutoka Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji na Jeshi la Magereza ili kubaini matatizo yao lakini kuweka pia mikakati ya kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi.
    Alisema si busara kwa wakuu wa vitengo na idara za Polisi, Uhamiaji na Magereza kutoshughulikia kero mbalimbali za watumishi, kwani kushindwa kufanya hivyo ni kuwasononesha askari ambao wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kupambana na majambazi na kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
    Alisema si vizuri kwa wakuu wa idara au vitengo ndani ya majeshi hayo, kutoshughulikia kero za watumishi wanaostahili kupandishwa madaraja, lakini pia kupewa motisha kwa kazi nzuri wanazofanya ikiwemo kupambana na majambazi.
    “Jamani shughulikieni kero za watumishi ambao ni hawa askari haiwezekani askari anapambana na majambazi halafu anaumia eti mnamuundia Tume kuchunguza tukio jinsi lilivyotokea tena Tume inaundwa na askari wenzie. Jamani hivi mtu amepambana na jambazi halafu kaumia au kupoteza maisha nyie mnazungusha mafao yake au motisha kwa kazi nzuri aliyoifanya?
    Hii haiwezekani. “Nawaomba sana pale tukio linapotokea na askari kaumia au kupoteza maisha kwa ajili ya kupigania nchi yake mumuangalie kwa jicho la pekee, ili kuondoa manung’uniko kwa polisi, lakini pia maslahi yao yaboreshwe zaidi. Ni vizuri sasa kwa wafanyakazi kuanisha vipaumbele vyenu kwa ajili ya mustakabali wa kulinda jeshi letu na kuboresha mambo mbalimbali,” alisema Waziri Mwigulu.
    Katika hatua nyingine, alisema hivi sasa serikali inaangalia kwa upekee suala zima la kuboresha makazi ya askari, hivyo ni vyema sasa wachora ramani za ujenzi wakachora ramani za kisasa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo za polisi kwa vile zilizopo hivi sasa hazikidhi mahitaji ya familia za askari kutokana na kujengwa katika mtindo wa kikoloni.
    Alisema kila mkoa uainishe ni nyumba ngapi zinastahili kujengwa na kwamba watatumia nguvu kazi ya Jeshi la Magereza ili kujenga nyumba mbalimbali nchini.
    Alisisitiza kuwa suala la ulinzi na usalama ni la kila raia, hivyo ni vyema kushirikiana na polisi ili kulinda usalama wa nchi pamoja na kufichukua wahalifu ili kudhibiti masuala ya ujambazi Akizungumza kuhusu kuongeza magari kwa ajili ya Jeshi la Zimamoto, alisema huo ni mkakati uliopo mbioni kwa ajili ya kupunguza madhara ya moto yanayoweza kutokea kutokana na majanga ya moto

    No comments:

    Post a Comment

    HABARI

    HABARI

    MICHEZO

    LOGO

    LOGO

    MAOJIANO

    BURUDANI