• Breaking News

    ..

    ..

    Monday, 22 August 2016

    Waziri Mkuu Majaliwa kuongoza harambee ya madawati


    WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye harambee ya kuchangia madawati iliyoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Ezekiel Kyunga kumaliza tatizo la upungufu wa madawati 68,459 kwa shule za msingi na sekondari mkoani hapa.
    Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Kyunga alisema harambee hiyo inatarajiwa kufanyika Agosti 27 mwaka huu. Maandalizi yake yamekamilika na matarajio ni kupata wadau wengi kutoka ndani na nje ya mkoa wa Geita.
    Alisema lengo la harambee hiyo ni kuchanga fedha kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi suala la uhaba wa madawati katika shule za msingi na sekondari ili watoto wote waweze kusoma wakiwa wamekaa katika madawati.
    “Kwa upande wa sekondari zinahitajika Sh bilioni mbili kwa ajili ya meza na viti na kwa shule za msingi zinahitajika Sh bilioni tano kwa ajili ya madawati. Hii itasaidia wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri ambayo yatafanya kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu katika shule zetu,” alisema.
    Alisema mkoa wake una jumla ya madawati 115,523 katika shule zote 571 za msingi na awali zenye wanafunzi 503,371 waliosajiliwa, kati yao wa darasa la kwanza wako wanafunzi 140,531 na zaidi ya wanafunzi 56,000 wameandikishwa katika wilaya ya Geita inayodaiwa kuvunja rekondi nchini ya uandikishaji darasa la kwanza.
    Lengo la mkoa ilikuwa kuandikisha wanafunzi 79,832 wa darasa la kwanza mwaka huu, lakini wamevuka lengo la asilimia 100 hadi kufikia asilimia 176.
    Kwa mujibu wa Mkuu wa mkoa Mkoa, unahitaji kuwa na madawati 183,982, lakini hadi kufikia Agosti 15 mwaka huu, mkoa ulikuwa umetengeneza madawati 115,523 ambayo ni sawa na asilimia 73, upungufu wa madawati uliopo ni 68,459 sawa na asilimia 37.
    Ametoa mwito kwa wadau wa Maendeleo kusaidia kuchangia madawati kupitia Akaunti ya Madawati Geita, CRDB 0150220596700, Benki ya Azania Na.0120121474023500 na NMB 31010018458

    No comments:

    Post a Comment

    HABARI

    HABARI

    MICHEZO

    LOGO

    LOGO

    MAOJIANO

    BURUDANI