WAKATI Tanzania leo inaungana na Jumuiya ya Kimataifa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni, serikali imewataka wafanyabiashara kuepuka kuingiza nchini gesi zilizopigwa marufuku na vifaa vinavyotumia gesi haribifu, kama vile majokofu na viyoyozi vilivyokwishatumika (mitumba).
Alisema viyoyozi na makojofu yanayotumia vipoozi aina ya R11 na R12, si rafiki kwa mazingira. Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba wakati akizungumza na vyombo vya habari na kusisitiza kuwa ni vyema wafanyabiashara wakawa makini ili kulinda mazingira ya nchi.
Akizungumzia maadhimisho hayo, January alisema yatafanyika kwa njia ya uelimishaji umma kuhusu Tabaka la Ozoni, faida zake, madhara ya kuharibika kwa tabaka na matumizi salama ya bidhaa zenye kemikali rafiki kwa Tabaka la Ozoni.
Alisema ni vyema wafanyabiashara wakaingiza nchini vipodozi mbadala na rafiki kwa tabaka la Ozoni kama vile R22, R134a, R407, R404 na R717 na kusisitiza kuwa kununua bidhaa zilizowekwa nembo rasmi isemayo “Ozone friendly” yaani “sahibu wa Ozoni” au “CFC-free” ikiashiria haina wala haikutengenezwa na kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni.
Aliwataka mafundi wa majokofu na viyoyozi wahakikishe wananasa na kutumia tena vipoozi kutoka kwenye viyoyozi, na majokofu wanayohudumia badala ya kuviachia huru visambae angani.
Aidha, mafundi watoe elimu kwa wateja wao juu ya njia rahisi za kutambua uvujaji wa vipoozi kutoka katika majokofu na viyoyozi wanavyotumia. Alisema pia elimu ya udhibiti wa kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Hewa ya Ozoni hiyo imetolewa pia kwa maofisa forodha na wasimamizi wa sheria 172 na kwamba hadi sasa Tanzania imepunguza zaidi ya tani 216 sawa na asilimia 86 ya kiasi cha matumizi ya kemikali hizo.
Akifafanua kuhusu maadhimisho hayo, alisema yanafanyika kutokana na agizo la Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Azimio lake nambari 49/114 la Desemba 19, 1998 kama kumbukumbu ya tarehe ya kutiwa saini Mkataba wa Montreal (Montreal Protocol - 1987) kuhusu kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Hewa ya Ozoni angani.
Alifafanua kuwa athari ya kuharibika kwa tabaka ni pamoja na kuchangia kuruhusu mionzi zaidi ya “Ultraviolet B” kufika kwenye uso wa dunia na hivyo kusababisha kuongezeka kwa magonjwa kama saratani ya ngozi, uharibifu wa macho yaani "mtoto wa jicho" unaosababisha upofu, upungufu wa kinga dhidi ya maradhi na kujikunja kwa ngozi.
Aidha, madhara mengine ni kuharibika kwa mimea hasa mazao ya kilimo kutokana na kuathirika kwa maumbile na mifumo ya ukuaji. Pia baadhi ya kemikali hizo zimetajwa kusababisha kuongezeka kwa joto duniani na hivyo kuchangia katika mabadiliko ya tabianchi.
No comments:
Post a Comment