• Breaking News

    ..

    ..

    Sunday, 18 September 2016

    Watoto wahamasishwe kupenda sayansi



    WAZAZI na walezi wameshauriwa kuwahamasisha watoto wao kupenda kusoma masomo ya hisabati na sayansi ili kuzalisha wataalamu wengi zaidi katika sekta hizo na hatimaye kukuza teknolojia nchini.
    Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Feza (Feza Boys), Ibrahim Yunus aliyasema hayo katika mashindano ya ‘Genius Cup’ yanayoendeshwa na shule hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) yaliyofanyika shuleni Tegeta, Dar es Salaam juzi.
    Yunus alisema kumekuwa na changamoto kubwa kwa wanafunzi wengi kuogopa masomo ya sayansi na hivyo kusababisha uhaba wa wataalamu wa sayansi nchini na hivyo kuendelea kudumaa kwa teknolojia.
    Alisema shindano hilo linalenga kuamsha ari ya wanafunzi wengi zaidi kupendelea kusoma masomo ya sayansi na hisabati ambapo kwa mwaka huu wanafunzi wa darasa la saba na wa kidato cha pili kutoka mikoa 10 nchini wameshiriki mashindano hayo.
    Alisema wanafunzi hao walipitia mchujo ambapo wanafunzi 63 walichaguliwa kuingia hatua ya mwisho ili kuopata washindi watatu.
    “Baada ya mchakato wa muda mrefu kwa sasa tumewaleta wanafunzi hawa Dar es Salaam kufanya mitihani ili tupate washindi watatu ambao watajinyakulia zawadi mbalimbali pamoja na fedha taslimu. Pia washindi hao wanasaidiwa kutimiza malengo yao,” alisema.
    Naye Ofisa Elimu Kata ya Mwasanga iliyopo mkoani Mbeya, Mwalimu Joshua Mwinuka alisema shindano hilo limekuwa likiibua vipaji vya wanafunzi na kuhamasisha wanafunzi wengi zaidi kupenda sayansi na hisabati ambapo kwa mwaka jana mkoa huo ulipata mshindi wa pili kwa shule ya msingi na mshindi wa pili kwa shule za sekondari.
    “Tunaomba shindano hili ikiwezekana lipelekwe mikoa yote ili kuhamasisha zaidi vijana wetu kupenda sayansi na hisabati kwa sababu kwetu tumeona manufaa yake. Mkoa wetu kwa mwaka huu hatua ya mwisho wameingia wanafunzi wane kutoka shule ya msingi na wawili kutoka shule za sekondari,” alisema.
    Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Seminari ya Mtwara Sisters, Hawa Mlowola alisema mashindano hayo yametoa fursa kubwa kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi na hisabati na kuwashauri wanafunzi wengine kutokata tamaa na kupendelea kusoma masomo hayo ambayo yana fursa nyingi za ajira.
    Walioibuka washindi katika mashindano hayo ni Roselyn Kissaka kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Feza aliyeibuka mshindi wa kwanza na mshindi wa pili akiwa ni Yokta Shreton wa Shule ya Sekondari Usanga ya Tanga na wa tatu ni David Praygod wa Shule ya Sekondari Famgi iliyopo mkoani Mwanza.

    No comments:

    Post a Comment

    HABARI

    HABARI

    MICHEZO

    LOGO

    LOGO

    MAOJIANO

    BURUDANI