SERIKALI imekiri kuwepo upungufu wa baadhi ya chanjo katika baadhi ya vituo vya kutolea huduma za afya.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema hayo leo wakati anazungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma kuhusu hali ya chanjo nchini.
Ametaja chanjo zilizopungua kuwa ni kwa ajili ya kukinga ugonjwa wa surua na rubella (MR), kifua kikuu (BCG), polio (OPV) na pepopunda (TT).
Kwa mujibu wa Ummy, chanjo hizo zinatumika kwa ajili ya watoto wanapozaliwa hadi miaka miwili na akinamama wajawazito kulingana na mwongozo wa chanjo, uliotolewa na wizara ili kuwakinga na magonjwa hayo.
Amesema, ili kukabiliana na upungufu huo, wizara imekwishanunua na inategemea kupokea chanjo ya polio dozi milioni mbili zitakazowasili Septemba 19, mwaka huu, chanjo ya pepopunda dozi 1, 240, 000 itakayowasili Septemba 26, mwaka huu na chanjo ya kukinga kifua kikuu kiasi cha dozi milioni mbili zitakazowasili Septemba 28, mwaka huu.
Amesema zitakapowasili, chanjo hizo zitasambazwa haraka nchi nzima kwa kutumia Bohari ya Dawa (MSD). Alitaja chanjo ambazo hazina upungufu kuwa ni chanjo za kukinga ugonjwa wa nimonia, chanjo ya kukinga kuharisha(Rotarix) na chanjo inayokinga magonjwa ya dondakoo, kifaduro, homa ya ini na homa ya uti wa mgongo na zinaendelea kutolewa kama kawaida katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Waziri Ummy alisema awali Hazina iliipa wizara Sh bilioni 1.6 kwa ajili ya chanjo za awali miezi mitatu, ambazo ndio zinatarajiwa kufika lakini Hazina imetoa tena Sh bilioni 6.1 kwa ajili ya ununuzi wa chanjo nyingine za surua na rubella na zinatarajiwa kutumwa na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto Duniani(UNICEF), ambao ndio wanunuzi wa chanjo hizo kwa niaba ya Serikali ya Tanzania. Katika mwaka huu wa fedha, serikali imetenga Sh bilioni 60 kwa ajili ya chanjo hizo.
Amesema licha ya uhaba huo wa chanjo, kuna baadhi ya wilaya chanjo ya aina moja haipo wakati wilaya nyingine zipo nyingi.
Ametaka waganga wakuu wa mikoa yote, kuhakiki takwimu za chanjo na kuzitawanya wilaya kwa wilaya ili kuhakikisha vituo vinapata chanjo zilizopo.
Amewahimiza wananchi hasa wazazi na walezi wenye watoto wa umri wa kupata chanjo, watakapopata taarifa ya uwepo wa chanjo zilizokosekana kuwapeleka mara moja watoto ambao hawakupata au hawajakamilisha chanjo kulingana na ratiba ili wakamilishe chanjo zao.
Vilevile kwa majeruhi ambao walikwenda vituoni na kukosa chanjo, nao waende vituo vilivyo karibu wakapate chanjo zao kulingana na walivyoandikiwa na madaktari.
Amewahakikishia wananchi kuwa huduma za afya zikiwemo chanjo, zinaendelea kutolewa nchini na hutolewa bure, waendelee kutumia huduma hizo wakati wote, kwani chanjo ni haki ya msingi ya kila mtoto.
No comments:
Post a Comment