SERIKALI imewataka baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), walioshirikiana na wenzao wa Mamlaka ya Mapato (TRA), kupitisha makontena zaidi ya 100 bila kukaguliwa na shirika hilo katika Bandari ya Dar es Salaam, kujisalimisha haraka.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki wakati akizindua Baraza la
Wafanyakazi wa shirika hilo. “Nimeanza kukusanya orodha ya majina ya watu waliosaidia kupitisha makontena haya na nikija nayo hawatapona,” alisema Mwijage.
Aliwataka wote wanaojijua kuhusika, kujisalimisha mapema na kutubu ili wasamehewe, kabla ya hatua hiyo. Makontena hayo yalipitishwa katika Bandari ya Dar es Salaam hivi karibuni bila ya kuthibitishwa na shirika hilo.
Waziri huyo pia aliitaka TRA kuacha kutoa makontena, bila ya shirika hilo kuthibitisha au kukagua ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini, kwa sababu mwenye mamlaka hiyo ni TBS.
Alisema watakaotubu kuwa walishiriki, waseme walishiriki vipi na lini, walishirikiana na nani na wataje sehemu yalikopelekwa makontena hayo ili serikali isaidie kukomesha hali hiyo.
Alisema anaamini kuwa waliofanya hivyo katika TRA, walifanya kwa utashi wao, bila ya ushiriki wa viongozi wao, na sasa wakati umefika wa kukomesha tabia hiyo.
Alhamisi iliyopita, Mwijage alitoa siku nne kwa wafanyabiashara waliopitisha makontena bandarini 100 bila kukaguliwa na TBS, wakatoe taarifa katika shirika. Alisema hayo baada ya kupata taarifa kuwepo kwa makontena 100, yaliyotolewa bandarini kwa siku zilizopita bila kukaguliwa na TBS.
“Nawataka wafanyabiashara wote waliochukua kontena hizo, wajisalimishe haraka TBS kabla ya kufika Jumanne ili wakaguliwe. Najua kuanzia kesho (Ijumaa) ni mapumziko, lakini TBS itaweka dawati la kuwasikiliza mpaka Jumatatu na ikifika Jumanne hatua zitachukuliwa kwa wahusika wote,” alisema Mwijage.
Alisema wafanyabiashara ambao hawatajisalimisha baada ya kumalizika kwa siku hizo hatua stahiki zitachukuliwa ikiwemo kulipa faini ya asilimia 15. TBS ni miongoni mwa wadau wa bandari.
Kutokana na huduma za shehena, bandari ina wadau wakuu ambao ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Forodha, Taasisi za kudhibiti ubora wa bidhaa, TBS, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume ya Kudhibiti Mionzi na nyinginezo.
Makontena hayo 100 yalipangwa kukaguliwa na TBS yakiwa katika Bandari Kavu (ICD), ambazo kwa mujibu wa taratibu, huhusika na kutunza mizigo inayoshushwa nchini.
Aidha, akizungumzia Baraza la Wafanyakazi, alilitaka baraza hilo kushirikiana na menejimenti kuhakikisha matatizo yanayojitokeza, yanapatiwa ufumbuzi kwa maslahi ya nchi na kwamba serikali itahakikisha inaongeza vitendea kazi na watumishi ili kufikia malengo ya shirika.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Egid Mubofu, baraza hilo lina wajumbe 48 wanaotoka katika vitengo mbalimbali na litakaa kwa muda wa miaka mitano.
“Baraza hili linaundwa kutokana na mkataba wa Menejimenti na Chama cha Wafanyakazi (RAAWU),” alisema Mubofu na kuongeza kuwa menejimenti itashirikiana na baraza kufanyakazi za shirika kwa tija.
Alisema wafanyakazi wanatakiwa kufanya kazi kwa weledi na uadilifu katika majukumu yao ya kila siku. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TBS, Profesa Makenya Maboko alilitaka baraza hilo kufanya kazi kwa kushirikiana na menejimenti na bodi kuhakikisha shughuli za udhibiti wa ubora zinafanyika kwa ufanisi. “Bodi itaendelea kuisimamia menejimenti na kuishauri ifanye kazi kwa kuzingatia sera na sheria,” alisema Profesa Maboko.
No comments:
Post a Comment