MKUU wa Wilaya ya Mkoani Hemed Suleiman Abdalla, ameelezea kuchoshwa na asasi za kirai, zinazobuni miradi ambayo inawanufaisha viongozi wake na kutaka kuanzisha miradi ambayo itawanufaisha wananchi wote .
Alisema ndani ya wilaya yake, zipo asasi kadhaa za kirai ambazo zinajishuhulisha zaidi kuomba fedha za wafadhili kwa ajili ya kunufaisha viongozi wake jambo ambalo haliwasaidii wananchi ambao ndio walengwa.
Mkuu huyo wa wilaya, alieleza hayo alipokua akizindua mradi wa mafunzo ya kuimarisha sera na sheria za mabaraza matano ya vijna ya wilaya hiyo, chini ya Jumuia ya JUKAVIPE , iliofanyika skuli ya Maendeleo ya sekondari Ngwachani.
Alisema , JUKAVIPE iliyoanzishwa miaka saba iliopita, imeshaleta matunda kwa wanajamii ya Pemba, ikiwa ni pamoja na kuwapa taaluma ya uoteshaji wa vitalu vya miche ya mikarafuu, na elimu ya uhifadhi wa mazingira.
Alisema kazi iliofanywa na JUKAVIPE, kama na asasi nyengine za kirai zingefanya kwa mujibu wa malengo na dhamira zao, zingeisaidia sana serikali katika kufikia malengo yake kwa wananchi.
“Mimi naielewa zvizuri JUKAVIPE, kwani imeshafanya makubwa kwa jamii, lakini zipo asasi nyengine kubwa, huomba fedha kwa wafadhili, na kujinufaisha wenyewe , bila kufanya waliokusudia’’,alifafanua.
Akizungumzia mradi wa mafunzo ya kuimarisha sera na sheria ya mabaraza ya vijana, Mkuu huyo wa wilaya, aliipongeza jumuia hiyo, kutokana na kufikiria jambo hilo.
Alisema mabaraza ya vijana yameanzishwa kwa lengo la kuwasomesha sera na sheria wajumbe wa mabaraza hayo matano na yatatoa mwanga kwa kuimarika kwa mabaraza hayo.
Nae Mwenyekiti wa JUKAVIPE, Ali Abdalla Said, alisema pamoja na kufanya vyema kwenye kazi, lakini changamoto makubwa zinazowakabili ni ukosefu wa ofisi ya kudumu.
“Hadi leo tunafanya kazi zetu kwenye nyumba ya mtu, ambapo tumekuwa tukipata usumbufu, maana raha ya shughuli kama hizi, uzifanye kwenye ofisi husika’’,alifafanua.
Mapema Mwakilishi wa Jimbo la Chambani Bahati Khamis Kombo, alisema yuko tayari kushirikiana na uongozi wa Jumuia hiyo wakati wowote, ili kufikia malengo yake.
Mbaraza ya vijana ya shehia ambazo zimebahatika kuingia kwenye mpango huo wa mafunzo ya kuimarisha sera na sheria ya baraza ya vijana chini ya JUKAVIPE, ni Ngwachani, Uweleni, Chumbageni, Jombwe na Mjimbini yote ya wilaya ya Mkoani Pemba.

No comments:
Post a Comment