KUSHAMIRI kwa ngoma za vigodoro katika wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro kumechangia kuwapo kwa mimba nyingi za utotoni ambazo ni tishio kwa maendeleo kielimu na kijamii.
Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe, alisema hayo juzi, alipokuwa akielezea changamoto zinazoikabili wilaya hiyo mbele ya Makamu wa Rais , Samia Suluhu Hassan, aliposimama kwa muda mjini hapo na kuzungumza na wananchi akiwa njiani kwenda Dodoma.
Mchembe, alisema mimba za utotoni katika wilaya hiyo zipo katika kiwango cha juu, zinachangiwa na ngoma za vigodoro, hivyo kuwafanya watoto wengi wa kike kukatisha masomo yao kutokana na kupata mimba na wengine kuzaa wakiwa na katika umri mdogo.
Hivyo alimwomba Makamu wa Rais, kutokana na fursa iliyopatikana na kuwepo kwake katika mji huo, azungumze na wazazi waliofika kumpokea kuhusu madhara ya mimba za utotoni.
Makamu wa Rais, alisikitishwa kuona watoto wadogo wa kike wanapata mimba wakiwa chini ya uangalizi na uzimamizi wa wazazi na walezi.
Hivyo alisema, kushamiri kwa mimba hizo za utotoni kunachangiwa na wazazi na walezi kushindwa kuwajibika ipasavyo katika malezi ya familia jambo ambalo linahatarisha maisha ya kielimu ya watoto hao.
“Vigodoro vinaandaliwa na sisi wazazi na walezi, na tunawaacha watoto wa kike na wavulana wakichezeana, lazima tuwadhibiti watoto wetu wa kike na wavulana katika jambo hili ili wapate maendeleo ya kielimu," alisema Makamu wa Rais.
Alisema, Serikali imeondoa ada kuanzia elimu ya awali, darasa la kwanza hadi kidato cha nne, ili kutoa fursa kwa watoto wote waweze kusoma bila vikwazo.
Hivyo, jukumu la wazazi na walezi ni kusimamia kwa karibu malezi ya watoto wao hasa wa kike ili wapate fursa ya kusoma kuanzia elimu ya awali hadi ya juu.
Makamu wa Rais, aliwataka wanafunzi wa kike kuzingatia falsafa ya uvaaji wa magauni manne ambayo ni sare ya shule, joho la mahafali, sare ya harusi na vazi la ujauzito na si kurukia vazi la ujauzito.
Aliagiza wazazi na walezi kuhakikisha mimba za utotoni katika wilaya hiyo, zinaondoka na kukomeshwa kabisa.
No comments:
Post a Comment