Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amewataka wataalam kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kutoa leseni kwa wakati kwa makampuni yanayojihusisha na shughuli za utafiti na uchimbaji wa gesi na mafuta nchini.
Profesa Muhongo aliyasema hayo jijini Dar es Salaam kwenye kikao cha majumuisho kilichoshirikisha makampuni yanayojihusisha na shughuli za utafiti na uchimbaji wa gesi na mafuta nchini, Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Mafuta (PURA). 

Alisema kumekuwepo na tabia ya ucheleweshaji wa uhuishaji wa leseni za utafiti na uchimbaji wa gesi na mafuta kwa makampuni yanayoomba leseni jambo linalokwamisha utendaji wa makampuni hayo.
Katika hatua nyingine, Profesa Muhongo aliyataka makampuni yanayofanya shughuli za utafiti na uchimbaji wa gesi na mafuta nchini kutuma maombi ya kuhuisha leseni zao miezi sita kabla ya muda wake kuisha.
Alisema kuwa biashara ya gesi na mafuta duniani ina ushindani mkubwa na kutaka kampuni za mafuta na gesi kuongeza kasi ya utafiti na watendaji kutoka TPDC na Wizara ya Nishati na Madini kuongeza kasi ya utoaji wa leseni.
Aliongeza kuwa mahitaji ya gesi yanazidi kuwa makubwa nchini kutokana na gesi hiyo kuhitajika majumbani, kwenye viwanda na kuzalisha umeme hivyo makampuni hayo yanatakiwa kuhakikisha kuwa gesi ya kutosha inayoendana na mahitaji halisi inapatikana.
Alisisitiza kuwa ili nchi ya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 nishati ya umeme wa uhakika inahitajika na kuongeza kuwa gesi ndiyo itakayochangia katika uzalishaji wa umeme wa uhakika.
Mkutano huu ulifanyika ukiwa ni moja ya utaratibu wa Waziri Muhongo kukutana na kampuni zinazojishughulisha na utafiti na uchimbaji wa gesi na mafuta kila baada ya miezi mitatu kwa ajili ya kujadili maendeleo ya shughuli pamoja na changamoto zake.

No comments:
Post a Comment