Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema ameshiriki katika zoezi la kugawa vyandarua kwa wananchi wa Kata ya Gerezani, akizungumza wakati wa zoezi hilo DC Mjema amewataka wananchi hao kuvitumia vyandarua hivyo kwa matumizi yaliyokusudiwa ili kuutokomeza kabisa ugonjwa wa Malaria.
DC Mjema ameeleza kuwa matumizi ambayo siyo sahihi kwa vyandarua hivyo ni kama kufugia kuku na kuvulia samaki jambo ambalo siyo sahihi kwani ni hatari kwa afya za familia husika, hivyo ameagiza wanaofanya hivyo wachukuliwe hatua kwa kwenda kinyume na maagizo ya serikali.
Pia DC Mjema amewapongeza wananchi wa Ilala kwa ujumla kwa ugonjwa wa Malaria kupungua kutoka asilimia 98 mwaka 2015 mpaka kufikia asilimia 7.1 kwa mwaka 2016 jambo ambalo limechochewa na kampeni ya kufanya usafi kila siku ya jumamosi na kuua mazalia ya mbu, ambapo amefafanua mpaka kufikia mwaka 2020 Malaria iwe imepungua mpaka asilimia 1.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala Victorina Ludovick ameeleza kuwa vyandarua hivyo vinatolewa bure na muitikio ni mkubwa kwani wamekwisha andikisha zaidi ya kaya 291,966 na idadi ya vyandarua ni 751,498 ambapo vituo vya ugawaji vipo 279 na kila kituo kina wagawaji wawili.
No comments:
Post a Comment