Mkurugenzi wa Idara ya Nyumba Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Michael Mwalukasa akizungumza na Waandishi wa Habari Leo Jijini Dar es salaam kuhusu mfuko wa kuwawezesha watumishi wa Serikali kumiliki Nyumba ambapo zaidi ya watumishi 2000 wameshanufaika na mikopo yenye riba nafuu ya asilimia 3 ili kuwawezesha kumiliki nyumba bora. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Mikopo ya Nyumba Bi Lucy Kabyemera na Kushoto
Mkurugenzi Msaidizi Mikopo ya Nyumba,Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi Lucy Kabyemera akifafanua kwa waandishi wa habari kuhusu faida wanazopata watumishi wa Umma kutokana na mikopo inayotolewa na Serikali ili kuwawezesha kumiliki makazi bora. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Nyumba Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Michael Mwalukasa.
Baadhi ya waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Leo Jijini Dar es salaam.
Picha na Frank Mvungi-Maelezo
……………………………………………………………………………………
Fatma Salum- MAELEZO
Serikali imewawezesha watumishi zaidi ya 2000 kumiliki nyumba bora kwa kuwapatia mikopo yenye riba nafuu na kuchangia kuongeza tija katika utumishi wa umma.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Nyumba Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. Michael Mwalukasa wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam.
Mwalukasa alisema kuwa kupitia Mfuko wa Mikopo ya Nyumba kwa Watumishi wa Serikali watumishi wengi walioomba mikopo hiyo wameweza kupewa kwa lengo la kuwawezesha watumishi wa Serikali wa ngazi zote mijini na vijijini kujenga, kukarabati au kununua nyumba.
“Mfuko huu umewawezesha watumishi wa Serikali kujenga nyumba kwenye maeneo yenye hadhi na yanayokubalika kisheria hivyo kuchochea kasi ya maendelezo ya nyumba kwenye Miji na Wilaya zote hapa nchini” alisisitiza Mwalukasa.
Akifafanua Mwalukasa amesema kuwa watumishi wanaokopa kwenye mfuko huo hurejesha mikopo hiyo kwa riba nafuu ya asilimia tatu tofauti na taasisi nyingine ambazo hutoza riba kubwa.
“Tofauti na taasisi nyingine ambazo hukopesha nyumba iliyokamilika na kutoza riba kubwa, mfuko huo unatoa mikopo kwa ajili ya kujenga,kununua na kuboresha nyumba na kuwapa fursa watumishi kukopa kadiri ya uwezo na matakwa yao ya ujenzi”. Alisema Mwalukasa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Mikopo ya Nyumba Bibi Lucy Kabyemera aliongeza kuwa baadhi ya wakopaji pia hunufaika na ushauri wa kutumia teknolojia ya gharama nafuu za ujenzi kutokana na tafiti zinazofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Vifaa vya Ujenzi wa Nyumba Bora (NHBRA).
Pia Kabyemera aliwataka watumishi wa Serikali kutumia fursa hiyo ili waweze kumiliki nyumba bora kwa gharama nafuu katika maeneo yaliyopimwa.
Mfuko wa Mikopo ya Nyumba kwa Watumishi wa Serikali ulianzishwa na Serikali mwaka 1963 kupitia waraka namba 8 na baadae kuendeshwa kupitia waraka wa watumishi wa Serikali namba 4 wa mwaka 1965.
No comments:
Post a Comment