• Breaking News

    ..

    ..

    Wednesday, 8 February 2017

    SERIKALI YAFAFANUA SHEREHE ZA MUUNGANO, GESI NA UENDESHAJI WA MICHEZO YA BAHATI NASIBU

    lude
    Dodoma, Jumatano, 8 Februari, 2017:  
    Serikali imefafanua kuhusu sherehe za Muungano, manufaa na kiasi cha gesi nchini na utaratibu wa michezo ya bahati nasibu hapa nchini. Ufafanuzi huo umetolewa leo mjini hapa.
    Zuio la Sherehe za Muungano
    Serikali imefafanua kuwa Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 52 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa mwaka 2016 yalifanyika kwa wananchi kupumzika siku hiyo na kuendelea kutafakari umuhimu wa Muungano. Alisema wananchi waliadhimisha kwa kufanya shughuli anuai kama vile usafi wa mazingira na kujitolea katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
    Akifafanua kuhusu hoja hiyo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Anthony Mavunde amesema si kweli kwamba sherehe hizo zilizuiwa na akaongeza kuwa Serikali haina kumbukumbu zozote za watu binafsi walioingia hasara kwa kufanya maandalizi ya sherehe hizo.

    Kiasi cha Gesi Nchini
    Serikali imesema kuwa gesi asilia iliyogunduliwa katika maeneo ya baharí ya kina kirefu ni futi za ujazo trilioni 47.08 na katika nchi kavu ni futi za ujazo trilioni 10.17, hivyo nchi kuwa na jumla ya futi za ujazo trilioni 57.25 za gesi asilia. Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani amesema gesi iliyogunduliwa nchini na safi ikiwa na kiwango kidogo cha kemikali ya alfa.
    Ameongeza kuwa moja ya manufaa ya gesi hiyo ni uzalishaji wa umeme ambapo mpaka sasa uzalishaji umeme kwa kutumia gesi asilia umeongezeka kutoka uniti 2,714.25 milioni kwa mwaka 2014 hadi uniti 4,196.4 milioni mwaka 2016 ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 54.61.
    Aidha, amesema kutokana na unafuu wa umeme wa gesi, bei ya umeme imeshuka kutoka wastani wa shilingi 188.56 kwa uniti mwaka 2014 hadi wastani wa shilingi 125.85 kwa uniti mwaka 2016 sawa na punguzo la asilimia 33.26.

    Ongezeko la Maduka ya Kucheza Kamari
    Serikali imefafanua kuwa, michezo yote ya kubahatisha ikiwemo kamari inapaswa kuendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Namba 4 ya mwaka 2003, Sura 41 pamoja na Kanuni zake. Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji amesema kwa mujibu wa Sheria, hakuna mtu au taasisi inayoruhusiwa kuendesha biashara ya Michezo ya Kubahatisha bila kuwa na leseni kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha.
    Dkt. Kijaji ameongeza kuwa Sheria pia inakataza watoto wenye umri chini ya miaka 18 kushiriki, kuingia, kukaa au kuzurura karibu na maeneo ya michezo ya kubahatisha. Ameasa kuwa, mtu yeyote atakaye ruhusu mtoto chini wa miaka 18 kushiriki, kuingia au kukaa karibu na eneo la mchezo wa kubahatisha anahesabuka kufanya kosa na anastahili kulipa faini ya sh. 500,000 au kifungo kisichopungua miezi mitatu ama vyote kwa pamoja.
    Imetolewa na:

    Idara ya Habari-MAELEZO.

    No comments:

    Post a Comment

    HABARI

    HABARI

    MICHEZO

    LOGO

    LOGO

    MAOJIANO

    BURUDANI