RAIS John Magufuli amesema kundi la majambazi linaloendesha mauaji mkoani Pwani hasa katika wilaya za Mkuranga na Kibiti halitapenya, bali litakamatwa kokote waliko.
Amesema amani ni jambo la msingi katika uwekezaji na akawataka wananchi kuwaambia ndugu zao ambao wanawafahamu kwamba wanafanya vitendo hivyo, kuacha mara moja.
“Hawatapenya, vyombo vya ulinzi na usalama viko imara, hapo walikuwa wanajaribu kupiga mruzi tu,” alisema Rais Magufuli jana asubuhi alipozungumza na wananchi wa Kijiji cha Mkiu Wilaya ya Mkuranga wakati wa kuweka jiwe la msingi la Kiwanda cha Vigae cha Good Will.
Alisema nchi inahitaji amani ili wawekezaji waje kwa wingi, kuwekeza miradi mbalimbali.
Alisema Mkoa wa Pwani umebadilika kutokana na viwanda vingi kujengwa mkoani humo na kusaidia kupunguza tatizo la ajira. “Wilaya ya Mkuranga peke yake ina viwanda 83, naambiwa Mkoa wa Pwani una viwanda zaidi ya 200, haya ndio maendeleo tunayotaka, akitokea mtu anahatarisha uwekezaji huu lazima tushughulike naye,” alisema Rais Magufuli.
Aliwahakikishia wawekezaji wa kiwanda hicho cha GoodWill Tanzania Ceramic Co. Ltd kuwa amani itakuwepo eneo hilo na wasifikirie kwenda kujenga viwanda vingine nje ya Tanzania, bali waendelee kujenga viwanda vingine vingi katika wilaya hiyo.
“Jengeni hapa viwanda vingi, bahati nzuri sisi ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC, soko la ukanda huu ni kama watu milioni 500, hivyo kuna uhakika wa soko la bidhaa zenu, hivyo jengeni viwanda vingi hadi huko baharini,” alisema Rais Magufuli.
Kiwanda cha Vigae cha Good- Will kinatumia gesi asilia na asilimia 95 ya malighafi ya kiwanda hicho, inapatikana eneo hilo na asilimia tano tu ndio inayoagizwa kutoka China.
Kina uwezo wa kuajiri watu kati ya 1,000 na 1,500. Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amesisitiza kwamba kama kuna wananchi wanasubiri chakula cha bure kupelekewa na serikali, watakufa kwa njaa kwani hakuna vya bure chini ya utawala wake.
“Hizi kauli zilizokuwa zinatolewa huko nyuma eti hakuna mwananchi atakayekufa kwa njaa, mimi siiungi mkono. Sasa nasema chini ya utawala wangu kuna watu watakufa kwa njaa wasipofanya kazi. Lazima tuambiane ukweli,” alisema Rais Magufuli
No comments:
Post a Comment