• Breaking News

    ..

    ..

    Friday 31 March 2017

    PEMBA:WANANCHI WAITAKA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA KUINGIZA KIPENGELE CHA WATOTO CHINI YA MIAKA 14

    DSC_4553
    Na Masanja Mabula –Pemba ..
    WANANCHI wa wilaya ya Mkoani , Mkoa wa Kusini  Pemba, wameitaka Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar, kuingiza kipengele cha watoto wanaoanzia miaka 14 kulipwa fidia, wakati wanapopata ajali wakiliokoa zao la karafuu.
    Walisema wachumaji wakubwa wa zao la karafuu ni watoto wenye umri kati ya miaka 14 hadi 17, hivyo ni vyema kwenye marekebisho ya sheria ya fidia, watoto wenye umri huo wakatambuliwa na sheria ili kulipwa fidia wanapopata ajali .
    Hayo walieleza  mbele ya Tume ya Kurekebisha Sheria, inayoongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Mshibe Ali Bakari, wakati ilipokutana na wananchi hao, ili kukusanya maoni yao, juu ya kuzifanyia mapitio sheria za usalama kazini na ile ya fidia zote za mwaka 2005.
    Maoni ya wananchi hao, yalikuja kufutia sheria ya sasa ya fidia ya mwaka 2005 kwamba, haimtambui kifidia kwa mtu aliyeanguka wakati akichuma karafuu, kama hajafikia umri wa miaka 18.
    Mjumbe wa mkutano huo Juma Bakar Shoka, alisema wachumaji hasa wa zao la karafuu ni watoto wenye umri kuanzia miaka 14 na kuendelea, hivyo lazima sheria iwatambue kulipwa fidia.
    “Mimi napendekeza kwenye sheria mpya ijayo ya fidia, na hawa watoto walipwe fidia, maana ndio hasa wenyewe wanaozichuma karafuu na hata skuli wakati mwengine hufungwa’’,alipendekeza.
    Nae Salum Omar alisema watu wenye umri mkubwa, wengi wao sio wachumaji hasa wa zao taifa la karafuu, na badala yake watoto wenye umri wa kati, ndio wahusika wakuu.
    “Hata mimi napendekeza sheria ya fidia ijayo, iwatambue watoto wenye umri kuanzia umri wa miaka 14 na kuendelea, maana tukifanya kinyume chake, tutawakosesha haki yao ya kujifunza kuchuma karafuu’’,alisema.
    Kwa upande wake Rashid Abdalla, alisema hata sheria inayokuja ielekeze wapi fedha hizo zinapatikana na kusiwe na urasimu, na kumfanya mpatwa na ajali kujuta kuzifuatilia.
    Akifungua mkutano huo Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar Jaji Mshibe Ali Bakar, alisema ingawa sheria za kimataifa zinakataza mtoto kufanyishwa kazi zenye kuhatarisha maisha yake, lakini hilo wataliangalia kwa ukaribu.
    Katika hatua nyengine Mwenyekiti huyo, alisema lengo la kuzifanyia marekebisho sheria za fidia na ile ya usalama kazini za mwaka 2005, kuhakikisha wananchi wote wanaishi kwa usawa.
    Sheria ambazo Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar inazifanyia mapitio ni ile sheria ya fidia ya kazini No 15 ya mwaka 1986 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2005 na sheria ya usalama kazini No 8 ya mwaka 2005.

    No comments:

    Post a Comment

    HABARI

    HABARI

    MICHEZO

    LOGO

    LOGO

    MAOJIANO

    BURUDANI