Mahojiano
NAPE Nnauye, jana ameondolewa kwenye
nafasi yake ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kufuatia
mabadiliko madogo yaliyofanywa katika Baraza la Mawaziri na Rais John
Pombe Magufuli.
Ingawa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania anayo mamlaka ya kufanya uteuzi wa nafasi yoyote wakati wowote
kwa mujibu wa katiba, tukio la kuondolewa kwa Nape, limepokewa kwa
mshtuko mkubwa na tasnia ya Habari nchini, hasa kwa kuwa alionekana
dhahiri kuwa pamoja nao katika kipindi hiki ambacho wametikiswa.
Nape, mtoto wa kada wa zamani wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) Brigadia Moses Nnauye, aliteuliwa katika Baraza la
Mawaziri la Kwanza la Rais John Magufuli Desemba 9, 2015 kushika wadhifa
huo. Hadi jana wakati akiondolewa ofisini, Nape anakuwa amehudumu
katika uongozi huo kwa siku 467, huku akionekana kama mtu ambaye
alitekeleza majukumu yake kwa namna ya kipekee, kwani kwa muda wote huo,
aliweza kukutana, kujadili na kutoa maamuzi mazuri kwa watu wote
waliohusika na wizara yake.
Ingawa wizara yake ilihusika na
wanamichezo, wasanii, wana utamaduni na wanahabari, lakini ni watu wa
kundi la mwisho ndilo waliopatwa na mshtuko mkubwa, hasa kwa kuangalia
siku zake tano za mwisho akiwa kiongozi, jinsi alivyoshirikiana nao
katika tukio kubwa na baya kuwahi kuitokea tasnia ya habari Tanzania.
Ijumaa ya Machi 17, 2017 usiku, chumba
cha habari cha televisheni ya Clouds kilivamiwa na askari, wakiongozwa
na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye alikwenda studio
na kuwatisha watangazaji, kwa kitendo chao cha kushindwa kurusha habari
iliyokosa vigezo, iliyomhusu Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima,
Josephat Gwajima.
Tukio hilo lilibakia kuwa siri ya kituo
hicho hadi video fupi ilipovuja, Jumapili Machi 19, 2017 na kuzua
mjadala mkubwa mitaani na kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, kitu
kilichomuibua Waziri Nape ambaye kupitia akaunti yake ya mtandao wa
Twitter, alisema kama Waziri anayehusika na habari, angekwenda kesho
yake, Jumatatu katika ofisi hizo ili kujua kilichotokea. Jumatatu ya
Machi 20, 2017 Waziri Nape alikwenda Clouds kama alivyoahidi na huko
akakutana na uongozi wa Clouds Media Group, chini ya Mkurugenzi wake
Mtendaji, Joseph Kusaga na kufanya mazungumzo.
Pia alikuwepo Mwenyekiti Mtendaji wa
kampuni za IPP, Reginald Mengi ambaye ni Mwenyekiti wa chombo cha
wamiliki wa vyombo vya habari, MOAT. Akionekana mtu aliyesikitishwa na
tukio hilo, Nape aliteua Kamati ya watu watano, ikiongozwa na Mkurugenzi
wa Idara ya Habari (Maelezo) Dk.
Hassan Abbas ili kutafuta ukweli wa tukio
hilo na kuwapa saa 24 ili wakamilishe ripoti yao. Jumanne, Machi 21
waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari walikusanyika Makao Makuu ya
Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) barabara ya Sam Nujoma kusikia
kilichosemwa na Kamati, lakini hakukuwa na chochote, kiasi kuzua
minong’ono kuwa ‘wakubwa’ wamezuia ripoti hiyo, jambo ambalo
lilikanushwa na Nape, aliyetaka kuwepo kwa subira, kwani kamati yake
ilikuwa bado kazini.
Jumatano, Machi 22, 2017 katika Ukumbi wa
Idara ya Habari (Maelezo) Waziri Nape alipokea ripoti ya kamati hiyo,
ambayo kabla ya kukabidhiwa, ilisomwa hadharani na Katibu wake, Deodatus
Balile. Akiipokea ripoti hiyo, Nape alisema imemsikitisha na akawataka
viongozi kuwa na ngozi ngumu, hasa wanapoongoza watu.
Alisema yeye sio mtu wa kutoa uamuzi juu
ya suala hilo, isipokuwa ripoti hiyo ataiwasilisha kwa mamlaka ya juu
yake, ambao ni Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, ambao ndiyo wenye mamlaka ya maamuzi.
Jumatano, Machi 23, 2017 taarifa
iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa ilisema
Rais John Magufuli amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri,
kwa kumteua Dk. Harrison Mwakyembe kuwa mbadala wa Nape, huku nafasi
yake yeye (Mwakyembe) ikichukuliwa na Profesa Paramagamba Kabudi. Maisha
kweli hayatabiriki, anyway, Karibu Mheshimiwa Harrison Mwakyembe,
uanzia pale alipoacha Nape Nnauye!
Share this:
No comments:
Post a Comment