TAARIFA YA WAZIRI WA AFYA,
MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO MHE. UMMY ALLY MWALIMU (MB)
KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI YA
MACHI 8, MWAKA 2017
Nchi yetu kama zilivyo nchi
nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa itaadhimisha Siku ya Wanawake
Duniani ambayo kilele chake kitakuwa tarehe 8 Machi, 2017 na kwa mwaka
huu itafanyika katika ngazi ya mkoa kwa kuzingatia amzingira ya mkoa
husika.
Aidha Kaulimbiu ya maadhimisho ya
mwaka 2017 ni “TANZANIA YA VIWANDA: WANAWAKE NI MSINGI WA MABADILIKO YA
KIUCHUMI”. Kaulimbiu hii imetoholewa kutokana na Kaulimbiu ya Kipaumbele
ya Umoja wa Mataifa mwaka huu katika Mkutano wa 61 wa Hali ya Wanawake
Duniani (CSW) inayosema “Women Economic Empowerment in the Changing World of Work” ambayo tafsiri yake kwa lugha ya kiswahili ni “Uwezeshaji Wanawake: Kiuchumi Katika Dunia ya Mabadiliko ya Kazi”.
Kaulimbiu hii ya “Tanzania ya
Viwanda: Wanawake ni Msingi wa Mabadiliko ya Kiuchumi” inalenga
kuhamasisha jamii, Asasi za Kiraia, Sekta Binafsi, Taasisi za Serikali,
Vyama vya Siasa, Wabia wa Maendeleo, mtu mmoja mmoja na wadau wengine
hapa nchini Tanzania kuongeza wigo wa fursa za kiuchumi kwa wanawake ili
kuwawezesha kushiriki na kunufaika na hatua za maendeleo katika kipindi
hiki ambapo Tanzania inaelekea katika uchumi wa kati na wa viwanda.
Chimbuko la kuanzishwa kwa Siku ya
Wanawake lilianza mwanzoni mwa miaka ya 1900 kufuatia maandamano ya
wanawake wafanyakazi wa sekta ya viwanda nchini Marekani kupinga
mazingira duni ya kazi. Waandamaji hao, walilalamikia ukosefu wa huduma
za kijamii na kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji katika ajira ikiwemo
wanawake kulipwa mshahara mdogo kwa kazi sawa ukilinganisha na wanaume.
Kwa kuzingatia hali hiyo, Umoja wa
Mataifa baada kuanzishwa mwaka 1945 uliridhia kuwa tarehe 8 Machi kila
mwaka iwe ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani. Uamuzi wa Umoja wa
Mataifa wa kuanzisha Siku ya Wanawake Duniani ulitokana na ukweli kwamba
masuala ya haki, maendeleo na usawa wa wanawake yalihitaji msukumo
maalumu na wa kipekee.
Lengo kuu la kuadhimisha Siku ya
Wanawake Duniani ni kutoa fursa kwa jamii kupima utekelezaji wa
maazimio, matamko, mikataba na itifaki mbalimbali za Kimataifa, kikanda
na kitaifa zinazohusu masuala ya maendeleo ya jinsia na uwezeshaji
wanawake. Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa haki za wanawake kiuchumi,
kijamii, kiutamaduni na kisiasa zinapatikana na zinalindwa.
Kuadhimisha Siku ya Wanawake
Duniani ni kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutambua na kuthamini
uwezo na mchango mkubwa wa wanawake katika kuleta maendeleo pamoja na
kuelezea jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali na wadau
mbalimbali katika kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kijamii ili waweze
kushiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo yao, familia zao, jamii
na Taifa kwa ujumla.
Aidha wanawake ni kundi kubwa na
muhimu katika jamii (asilimia 51 ya Watanzania Wote) na kwamba hakuna
maendeleo yeyote yanayoweza kufikiwa ikiwa kundi hili litaachwa nyuma.
Kwa mantiki hiyo, Serikali kwa
kushirikiana na wadau imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika
kuhakikisha wanawake wanashiriki na kunufaika na uchumi hasa katika
kipindi hiki ambacho nchi yetu imejipanga kuelekea katika uchumi wa
viwanda na kuwa nchi ya uchumi wa kati.
Taarifa ya Jukwaa la Uchumi
Duniani kuhusu ‘Pengo la Jinsia ya Mwaka 2016’ inaonesha kuwa kutokana
na jitihada zilizofanyika nchi yetu inashika nafasi ya 53 kati ya nchi
144 zinazofanya vizuri katika masuala ya jinsia Duniani.
Katika jitihada za kuwawezesha
wanawake kiuchumi Serikali imeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake
ambao unatoa mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya kuwawezesha
wanawake wajasiriamali wadogo kuanzisha na kuendeleza biashara, viwanda
vidogo, kilimo pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi.
Aidha kupitia Mfuko huo,
Halmashauri zimehamasishwa kuchangia asilimia tano ya mapato yao ya
ndani ambapo katika kipindi cha Julai hadi Disemba, 2016 kiasi cha shs.
4,102,808,513 kilitolewa kwa vikundi vya wanawake na vijana katika
Halmashauri 101 kupitia utaratibu huu.
Benki ya Wanawake Tanzania pia
ilitoa mikopo yenye thamani ya Shs 9,323,240,000/- kwa wajasiriamali
6,267 kati ya hao wanawake walikuwa 4,596. Hivyo, kiasi cha mikopo
iliyotolewa imeongezeka kutoka Tshs. 112,473,600,000/- mwaka 2015 hadi
kufikia Shs 121,796,840,000/- mwaka 2016.
Aidha, idadi ya wajasiriamali
waliopata na kunufaika na mikopo inayotolewa na Benki ya Wanawake
Tanzania iliongezeka kutoka wajasiriamali 79,983 mwaka 2015 hadi kufikia
wajasiriamali 86,250 mwaka 2016 ambapo asilimia 73 ya wanufaika wa
mikopo hiyo ni wanawake.
Kwa kutambua umuhimu wa ushiriki
wa wanawake katika fursa mbalimbali za kiuchumi, Serikali imeratibu na
kuzindua majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi. Majukwaa haya
yatatumika kama sehemu muhimu kwa wanawake wajasiriamali kukutana na
kujadili fursa za kiuchumi pamoja na changamoto mbalimbali
zinazowakabili na namna bora ya kukabiliana na changamoto hizo.
Aidha, sheria ya Utumishi wa Umma
ya Mwaka 2002, (ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2007) imetoa fursa sawa
za ajira kati ya wanawake na wanaume. Kwa mujibu wa Sheria hiyo, pale
inapotokea mwanaume na mwanamke wanapata alama sawa wakati wa usaili,
mwanamke anapewa kipaumbele kupata nafasi hiyo.
Sheria ya Kazi na Mahusiano Kazini
(2004) imetoa fursa sawa kati ya wanawake na wanaume kuhusu haki zao za
ajira, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa likizo ya uzazi kwa wanawake na
wanaume.
Kwa kutambua elimu na mafunzo ni
nyenzo muhimu katika kuhakikisha wanawake na wanaume wanashiriki na
kunufaika ipasavyo na uchumi wa viwanda, Serikali imeendelea kuhakikisha
kila mtanzania anapata elimu kama haki ya msingi.
Katika kuhakikisha kuwa mtoto wa
kike na wa kiume wanapata haki ya elimu, Serikali inatekeleza sera ya
Elimu bila malipo ambayo inatoa fursa ya Elimu ya Msingi na ya Sekondari
na kuwahakikishia watoto elimu hiyo bila kujali tofauti za kiuchumi.
Sera hii imeleta mafanikio makubwa
katika eneo hili ambapo takwimu zinaonesha kuwapo ongezeko la udahili
kwa watoto wa kike na kiume
Pamoja na masuala yote yaliyotajwa
hapo juu Kumekuwepo na ongezeko la ushiriki wa wanawake katika ngazi
mbalimbali za maamuzi. Marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1995 na ya mwaka 2005 yalifanywa na kuongeza idadi ya
viti maalum kwa wanawake vilivyoongezwa hadi kufikia asilimia 30.
Katika kuhakikisha kuwa wanawake
wanajengewa uwezo wa kisheria na kupata haki zao, sheria kadhaa
zimetungwa na nyingine kufanyiwa marekebisho ikiwemo Sheria ya Makosa ya
Kujamiiana yaani (SOSPA) ya mwaka 1998, ambayo imefanyiwa marekebisho
na kuhuishwa kwenye Sheria ya Kanuni za Adhabu.
Sheria ya Ajira na Mahusiano
kazini Na. 6 ya mwaka 2004 ambayo imetoa fursa sawa katika ajira na
likizo ya Uzazi pamoja na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009; Sheria ya Ardhi
na Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999, ambapo sheria hii inampa
mwanamke haki ya kumiliki na kurithi ardhí sawa wanaume.
Pia, katika mwaka 2016/17 Bunge la
Jamhuria ya Muungano limepitisha Sheria ya Msaada wa Sheria ya mwaka
2016 ambayo itasawadia wanawake hasa wenye kipato cha chini kupata haki
zao za msingi.
Serikali inatambua kuwa ukatili
dhidi ya wanawake bado ni tatizo kubwa ambalo linaathiri ushiriki wao
katika shughuli za kiuchumi na kijamii. Katika kukabiliana na
tatizo hilo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa
Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto
(2017/18 – 2021/22) ambao ulizinduliwa tarehe 13 Disemba, 2016.
IMETOLEWA NA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO
No comments:
Post a Comment