• Breaking News

    ..

    ..

    Saturday 29 April 2017

    KUHUSU ZOEZI LA USAFI OFISI KUU BUGURUNI KESHO TAREHE 30/4/2017:



    Jana Tarehe 28/4/2017 Tumepokea barua kutoka Jeshi la Polisi Wilaya ya Buguruni yenye Kumb: BUG/SO.7/2/VOL.II/122 ya Tarehe 27/4/2017 ikishauri na kuzuia wanachama wa CUF kufanya usafi uliokusudiwa kwa hoja ya uvunjifu wa Amani.

    Barua hiyo iliyosainiwa na TARAJA C.CIBE-SSP, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Buguruni na baadae taarifa ya barua hiyo kutangazwa na Kamishna wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Ndugu. SIMON SIRRO mbele ya waandishi wa habari.

    Leo tarehe 29/4/2017 kilifanyika kikao cha mashauriano baina ya Wabunge, Wakurugenzi wa Chama, na Kamati ya Uongozi Taifa na iliazimiwa kwenda kumuona Kamishna Sirro.

    Kamati ya Uongozi ya Taifa chini ya Mwenyekiti wake MHE.JULIUS MTATIRO imechukua hatua za makusudi kuwasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini - IGP ili kuhakikisha kuwa usafi huo unafanyika kwa njia ya Amani.

    Baada ya mawasiliano na majadiliano hayo: Jeshi la Polisi limeahidi kuchukua hatua za kuwadhibiti Wahalifu wote ambao wamekuwa wakiitumia Ofisi Kuu ya CUF Buguruni kuratibu vitendo vya Kijinai na hivyo kuichafua kwa kila hali.

    Pia, jeshi la Polisi limeomba lipewe muda zaidi kuchunguza na kushughulikia matukio ya hivi karibuni na liweze kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watu wote waliopanga njama za uvamizi wa viongozi na wana habari pale Vina Hotel ikiwemo kumsaka mtu aliyekuwa na Bastola.

    Jeshi la Polisi limewahakikishia viongozi wa CUF kuwa litatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na hivyo lingependa kwanza kukijua vizuri kikosi cha "Mazombi" wanaotumwa kupiga na kuumiza viongozi wa chama na hivyo chama kisitishe matukio makubwa yanayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.

    Kutokana na makubaliano ya utekelezaji wa pande zote mbili (Jeshi la polisi na Uongozi wa CUF), KAMATI YA UONGOZI YA CUF - Taifa imeona ni busara kutoa muda zaidi kwa Jeshi la Polisi kuchukua hatua walizojiwekea juu ya masuala yaliyojitokeza na hivyo kuwaomba Wanachama na Viongozi wote kukubaliana na kuahirisha zoezi la kufanya Usafi katika Ofisi yetu ya Buguruni kesho Jumapili tarehe 30/4/2017 kama ilivyokuwa imepangwa.

    Mimi kama mratibu za zoezi hilo na kwa niaba ya wanachama wa CUF wilaya ya Temeke ambako mimi ni mbunge, nimeridhishwa na maelekezo haya ya viongozi wangu wa juu na nawaomba sote tuyakubali, walau kwa kipindi hiki.

    Tunawapongeza Wanachama, wapenzi wa CUF, Wabunge na Viongozi wote wa CUF walioonyesha utayari wa hali na mali na kwenda kufanya usafi katika Ofisi yao. Pale itakapojidhihirisha kuwa hakuna hatua stahiki zinazochukuliwa na Jeshi la Polisi, Viongozi wa CUF hawatasita kuwajulisha wanachama wake kuchukua hatua kwa gharama yeyote ile.

     

    HAKI SAWA KWA WOTE


    ……………………………………………………..
    ABDALLAH MTOLEA(MB-TEMEKE)
    NAIBU MKURUGENZI WA MAMBO YA NJE
    NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

    Imetolewa leo Tarehe 29/4/2017

    No comments:

    Post a Comment

    HABARI

    HABARI

    MICHEZO

    LOGO

    LOGO

    MAOJIANO

    BURUDANI