KUHUSU UVAMIZI NA UHALIFU WA KIJINAI ULIOFANYWA NA KUNDI LA LIPUMBA KWA MWENYEKITI WA WILAYA YA KINONDONI NA MJUMBE WA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA MHE. JUMA MKUMBI:
Leo Tarehe 22/4/2017 Mhe. Mkumbi aliandaa mkutano na waandishi wa habari katika ukumbi wa Vinna Hotel iliyopo Mabibo, Dar es Salaam. Mhe Mkumbi ameitisha mkutano huo akiwa ni Kiongozi Mkuu wa shughuli za Chama wilaya ya Kinondoni ili kuzungumzia masuala mbalimbali yaliyojitokeza katika Wilaya yake baada ya kuwa nje ya nchi nchini Marekani kwa wiki kadhaa. Wakati anaendelea na Mkutano wake ghorofa ya nne (4th Floor) na waandishi wa habari takribani 25 kutoka vyombo mbalimbali vya habari ghafla kundi la wafuasi wa Lipumba walifika Hotelini hapo wakiwa na gari mbili za Chama cha CUF Land Cruiser zilizokuwepo Ofisi Kuu-Buguruni huku wakiwa wameficha sura zao kwa Soksi, wameshika silaha mbalimbali ikiwemo mapanga na mmoja akiwa na bastola na kuanza kuwashambulia waandishi wa habari na Viongozi wa CUF waliokuwepo katika mkutano huo. Katika kujitetea wa walinzi wa Chama pamoja na wananchi waliojitokeza kuwashambulia wavamizi hao ndipo walilazimika kukimbia kwa kupanda magari waliokuja nayo na wananchi walifanikiwa kumkamata mmoja wa mfuasi wa Lipumba waliofanya uvamizi na kumjeruhi vibaya miguuni na sehemu ya kichwani. Viongozi wa CUF walizuia wananchi wenye hasira wasimchome moto muhalifu huyo, hata hivyo Wananchi waliendelea kuwashambulia wahalifu na kuvunja vioo vyote vya magari hayo na kukimbia. Waandishi wote waliojeruhiwa wametoa maelezo yao kituo cha Polisi Magomeni.
MSIMAMO NA TAMKO LA CHAMA CUF JUU YA TUKIO HILO:
1. CUF Tunalaani vikali kitendo hicho kilichofanyika na kundi la Lipumba kwa uratibu wa Abdul Kambaya, BG Fadhili na Masoud Mhina kwa Baraka zote Profesa Ibrahim Lipumba. Kitendo hicho si cha kiungwana na hakiashirii nia njema, uvumilivu na uendeshaji wa siasa za kistaarabu. Kama Katibu wa Wilaya Mzee Mkandu juzi tarehe 19/4/2017 alifanya Mkutano kama huo kwa amani bila bughudha na watanzania walisikia alichokizungumza, iweje Mwenyekiti wake wa Wilaya ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa afanyiwe vurugu hizo?
2. Iweje Jeshi la polisi Limuachie Lipumba kuratibu kundi la wahalifu bila ya kuchukuliwa Hatua za kisheria? Hivi hata kama mathalani mkutano ule haukuwa halali, hii ndio njia sahihi ya kuzuia kutofanyika kwake? Iweje Jeshi la Polisi linabariki kitendo cha uharibifu wa mali za raia mwema mfanyabiashara wa Hotel ambaye analipa kodi kwa serikali huku ikiacha kuwachukulia hatua zinazostahiki wahalifu hao?
3. Tunatoa pole kwa waandishi wote wa habari waliojeruhiwa katika tukio hili linalopaswa kulaaniwa na kila mpenda haki na demokrasia nchini na CUF itaendelea kuwa pamoja nanyi kuhakikisha kuwa mnarejea katika hali yenu njema ya afya ili kutekeleza majukumu yenu ya kuwatumikia Watanzania.
4. Tunalitaka Jeshi la Polisi Mkoa wa Dar es Salaam kuwakamata wahusika wote wa tukio hilo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria (mahakamani). Matukio kama haya yanayofanya na kundi la llipumba yamekuwa yakijirudia mara kwa mara ikiwemo jaribio la Utekaji kwa Kaimu Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara Mhe. Joran Bashange mbali na wahusiaka wanne (4) kukamatwa eneo la tukio lakini Tunasikitika kuona Jeshi la polisi Mkoa-ZCO, na DPP wamekalia mashtaka hayo na kushindwa kuchukua hatua za kisheria. Tunalitahadharisha Jeshi la Polisi kutekeleza wajibu wao wasusibiri machafuko na maafa makubwa zaidi yatokee. Na orodha ya matukio hayo tumeiambatanisha na taarifa hii.
5. Tunamtahadharisha Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Franscis Mutungi na Profesa Lipumba kuwa wao watawajibika juu ya athari na machafuko makubwa zaidi ikiwemo mauaji yatakayojitokeza kwa kushindwa kuheshimu sheria na kuchochea ufanyikaji wa vurugu hizi. Lipumba amekne ya kufanya.
6. Mheshimiwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), hakuna maslahi yeyote unayoweza kuyapata kwa kuendelea kubariki ufanyikaji wa vitendo hivi vya uvunjifu wa amani katika nchi yetu zaidi ya kuendeleza kujengwa Chuki zaidi kati ya Jeshi la Polisi na raia wema, wananchi pale linaposhindwa kuwatendea haki wananchi wote kwa usawa. IGP chukua hatua utasababisha mauaji. Kwa kuwalinda wahalifu.
7. Tunatoa wito kwa Jukwaa la Wahariri wa Habari nchini kuchukua hatua dhidi ya Lipumba na kundi lake ambao sasa wamehamia kuwadhuru waandishi wa habari na kutoa lugha za vitisho pale zinaporipotiwa taarifa kinyume na matakwa yao. Baada ya kuendesha vitendo hivi kwa muda mrefu sasa kwa viongozi na wanachama wa CUF wakati mwingine ndani ya Mahakama Kuu.
HAKI SAWA KWA WOTE
MBARALA MAHARAGANDE
NAIBU MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI
NA MAHUSIANO NA UMMA
MAWASILIANO:
0784 001 408 Airtel | 0767 062 577 Vodacom
Imetolewa Leo Tarehe 22/4/2017
ORODHA YA MATUKIO JESHI LA POLISI KUINGILIA SHUGHULI ZA KISIASA ZA CUF;
Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharifu Hamad akiongea na waandishi wa Habari Peacock Hotel November, 2016 alieleza matukio kadhaa jinsi Jaji Francis Mutungi Jeshi la Polisi, na Lipumba wanavyoshirikiana katika kuhakikisha kuwa hujuma zinazofanywa dhidi ya Chama cha Wananchi (CUF) zinafanikiwa. Mtiririko wa matukio yafuatayo unaonesha wazi hujuma hizo ambazo mpaka leo hakuna hata moja ambayo Jeshi la Polisi imeifikisha Mahakamani;
1. KUVAMIA NA KUSABABISHA VURUGU ZISIZO ZA LAZIMA KATIKA MKUTANO MKUU MAALUMU WA TAIFA WA CUF, ULIOFANYIKA BLUE PEARL HOTEL, UBUNGO PLAZA, TAREHE 21 AGOSTI 2016 Chama kilitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi Kituo cha Magomeni lakini hakukuwa na hatua zozote zilizochukuliwa mpaka sasa zaidi ya kupewa RB namba MG/RB/9072/2016 ya tarehe 22 Agosi 2016.
2. UTEKAJI WA WANACHAMA NA VIONGOZI WA CUF; Tarehe 16 Septemba 2016, Kaimu Naibu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wetu wa Uchumi na Fedha Mhe. Joran Bashange alitekwa akitoka nyumbani kwake Mtaa wa Madenge, Buguruni, Wilaya ya Ilala. Walinzi wa Profesa Lipumba wanaofahamika kwa majina, sura, mahali wanapoishi na shughuli wanazofanya, walimvamia, wakamkamata na kumuingiza kwa nguvu kwenye gari aina ya Toyota NOAH yenye namba za usajili T760 CEX. Watuhumiwa wane (4) walikamatwa eneo la tukio na gari lao na kuwapeleka Kituo cha Polisi Buguruni. kesi Namba BUG/IR/5937/2016 la tarehe 16 Oktoba, 2016 lakini hakuna hatua yoyote muhimu iliyochukuliwa na Jeshi la Polisi. Jeshi la Polisi na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wameshindwa kuchukua hatua zinazostahiki dhidi ya uhalifu huo uliomlenga kiongozi wa ngazi za juu wa Chama cha Wananchi – CUF. Kinyume chake Jeshi la Polisi limewafikisha mahakamani kwa kuwabambikizia kesi ya jinai namba 354/2016 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, vijana 23 walinzi wa CUF (Blue Guard). Kwa kuwa tu vijana hawa hawamuungi mkono Profesa Lipumba.
3. UVAMIZI WA AFISI KUU YA CHAMA BUGURUNI DAR ES SALAAM, TAREHE 24 SEPTEMBA, 2016: Tarehe 24/9/2016 Prof Lipumba na wafuasi wake walivamia Ofisi Kuu ya Chama iliyopo Buguruni, Wilaya ya Ilala Mkoa wa Dar es Salaam kuvunja mageti na milango ya ofisi, kuwapiga walinzi binafsi wa Kampuni ya Ironsides Security Guard, kuwanyanganya silaha na kufanya uharibifu mkubwa wa mali za Chama. Hata hivyo taarifa ya uhalifu huo ilitolewa na walinzi wa Kampuni ya ulinzi ya Ironsides na kupewa RB Na.BUG/RB/8741/2016 ya tarehe 24 Septemba 2016 lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa mpaka sasa dhidi ya watuhumiwa. Jeshi la polisi ndio lilikuwa linamlinda Lipumba na watu wake.
4. UVAMIZI NA KUVUNJA OFISI ZA WILAYA BAGAMOYO NA MKURANGA: Tarehe 4 Novemba 2016 Profesa Lipumba na wafuasi wake wakilindwa na Jeshi la Polisi walikwenda Ofisi za Chama za Wilaya ya Bagamoyo. Tarehe 24 Septemba 2016, Jaji Francis Mtungi aliandika barua nyingine kwa Profesa Lipumba yenye Kum.Na.HA.322/362/14/88 ya tarehe 28/9/2016 na kuinakili rasmi kwa IGP ambayo ndiyo inatumika kumhakikishia ulinzi kwa uhalifu unaoendelea sasa.
5. WABUNGE NA WAJUMBE WA BARAZA KUU LA UONGOZI CUF TAIFA KUZUILIWA KUFANYA KIKAO CHA NDANI NEWALA NA KUKAMATWA NACHINGWEA: Wakati jeshi la polisi likimpa ulinzi profesa lipumba kufanya shughuli za kisiasa, maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo Mtwara Mjini, Newala, Nachingwea, Lindi, Tabora, Kahama, Bagamoyo, Mkuranga, Kisarawe, Morogoro, Kondoa na kwingineko. Tarehe 15 Oktoba, 2016 siku chache baada ya ziara ya profesa lipumba Jeshi la Polisi hao hao wakiwa na mabomu ya machozi na silaha za moto walivamia na kuwazuia wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na wabunge wa CUF, kufanya kikao cha ndani wilayani Newala na kuwatawanya wajumbe wote waliohudhuria. Jeshi la Polisi halikutoa sababu za kuvamia kufanya hivyo. Tarehe 16 Oktoba, 2016 Jeshi la Polisi lilizuia vikao vya ndani kwa wajumbe hao Kufanyika Mtwara Mjini. Wakiwa Nachingwea Jeshi la polisi liliwakamata wajumbe wa Baraza Kuu na wabunge na kuwaweka ndani kwa mahojiano na baadae kuwaachia na kuzuia kufanya shughuli yeyote ya kisiasa ndani ya wilaya hizo.
6. KUZUIA KUFANYIKA KWA MKUTANO MKUU MAALUMU WA WILAYA YA TANGA TAREHE 29/10/2016: Tarehe 29/10/2016 Uongozi wa wilaya ya Tanga ulimualika Katibu Mkuu, Maalimu Seif kuhudhuria ufunguzi wa Mkutano wao Mkuu Maalumu wa Wilaya, Jeshi la Polisi bila ya sababu za msingi na kuingilia majukumu ya kiutendaji kisiasa. Wakazuia kufanyika kwa mkutanoo huo.
7. UTEKAJI WA MLINZI WA CHAMA ULIOFANYIKA MAHAKAMA KUU TAREHE 10/11/2016: Mohamed Said PF3 kwa ajili ya matibabu na kufunguliwa jalada Na.CD/CID/PE/88/2016 la tarehe 10/11/2016, lakini hadi sasa hakuna taarifa wala juhudi za Polisi kuwakamata watuhumiwa ambao wote wapo Ofisi za Chama Buguruni wanakokaa kwa mabavu na kupewa msaada wa kiusalama na Jeshi la Polisi.
8. KUHUSU JESHI LA POLISI KUZUIA KUFANYIKA KWA KIKAO CHA NDANI MKOANI MTWARA NA LINDI: tare 19 na 20 Novemba, 2016 kilichopangwa kuhudhuriwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif. Lakini Lipumba anapewa ulinzi hata pale wanachama wasipomtaka na kumzomea kama Ruangwa bado Jeshi la Polisi Lilimlinda. Na kulazimisha kikao kufanyika.
9. WALINZI WA PROFESA LIPUMBA KUTAKA KUZUIA VIONGOZI WA CUF WASIINGIE NDANI YA CHUMBA CHA MAHAKAMA KUFUATILIA SHAURI na kuwajeruhu wanachama kwa visu wakiwa ndani ya Mahakam kuu – dar es salaam.
10. Jeshi la Polisi Kuwazuia Wakurugenzi wa Chama na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kuhudhuria na kufanyika kwa mkutano mkuu wa wilaya ya Ruangwa Tarehe 25/3/2017.
11. Jeshi la Polisi Kuzuia Mbunge wa Temeke MHE. Abdallah Mtolea ambae pia ni NAibu Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kukutana na wanachama na wananchi wake kesho tarehe 23/4/2017 huku Lipumba wakimlinda na Kufanya vikao.
Orodha ya matukio ya uhalifu na hujuma dhidi ya Chama chetu ni ndefu na si kazi rahisi kuielezea yote.
Maharagande,
22/4/2017

No comments:
Post a Comment