WABUNGE walionufaika na mikopo iliyotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuanzia mwaka 1994 wametakiwa kujisalimisha na kuanza kulipa marejesho.
Agizo hilo limekuja baada ya HESLB kupeleka barua Ofisi ya Bunge inayowataka wabunge walionufaika na mikopo hiyo kuanza kujiorodhesha na kuanza kurejesha fedha hizo.
Akisoma tangazo hilo bungeni jana, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, aliwaambia wabunge hao kuwa watumishi wa Bunge wataanza kugawa fomu ili kila mbunge aanze kujiorodhesha.
Novemba 14, mwaka jana, HESLB kupitia Mkurugenzi wake, Abdul-Razaq, ilitoa notisi ya siku 30 kwa wadaiwa sugu wa mikopo wawe wameanza kulipa madeni yao kabla hatua zaidi hazijachukuliwa.
Notisi hiyo ilieleza kuwa inawalenga wanufaika waliokopeshwa na muda wa marejesho ukapita bila wao kuwasilisha taarifa zao.
Katika operesheni waliyoiendesha tangu kutolewa kwa notisi hiyo, wanufaika 93,500 walibainika na kupelekewa ankara ya madeni yao ili waweze kulipa.
Hata hivyo, HESLB ilikusanya Sh bilioni 25 zilizorejeshwa kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 kwa wadaiwa 81,085, huku wadaiwa sugu 142,470 wenye mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 239 hawajajitokeza wala kuanza kulipa mikopo yao.
Jana, Dk. Tulia alisema wabunge ambao kwa nyakati tofauti walikuwa ni wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu iliyotolewa kuanzia mwaka wa masomo wa 1994/1995 wanapaswa kujisalimisha.
“Ofisi ya Katibu wa Bunge inawaomba wabunge wote kujihakiki ikiwa miongoni mwenu wapo waliokuwa wanufaika na mkopo huo lakini hawajaweza kurejesha fedha walizokopeshwa na bodi,” alisema.
Dk. Tulia alisema utaratibu wa uhakiki huo unafanyika kwa kuwa wabunge wengi kabla ya Novemba, mwaka juzi walikuwa katika majukumu mengine ya kikazi na kusababisha makato ya mikopo kusimama na kuonekana kama wadaiwa sugu, jambo ambalo si sahihi.
“Tafadhali mnatakiwa kujihakiki kwa kujaza fomu zilizoambatanishwa na dokezo hili, hivyo vijana wetu watawaletea fomu ili mjiandikishe na wabainike wale wanaodaiwa, hata mimi nilikuwa ni mdaiwa lakini nimelipa deni lote,” alisema.
Dk. Tulia alisema umuhimu wa kujihakiki utawasaidia wabunge ambao hawajarejesha mikopo ya elimu ya juu kuondokana na usumbufu usio wa lazima, ikiwamo kuchukuliwa hatua za kisheria na kudhalilika na kufikishwa mahakamani
No comments:
Post a Comment