Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna
Mstaafu Zelote Stephen amewataka wale wote wanaohusika na usimamizi wa
fedha za ukarabati wa moja ya shule Kongwe nchini, kuhakikisha kuwa
fedha hizo zinatumika kama zilivyokusudiwa.
Ameyasema hayo baada ya
kuzungukia maeneo yote ya shule yanayoendelea kukarabatiwa wakati
alipofanya ziara ya kushtukiza ili kujionea hatua waliyofikia katika
ujenzi na kutathmini kama thamani ya pesa inakwenda sambamba na ujenzi
unaoendelea katika shule hiyo.
Shule ya Sekondari ya Kantalamba
ni miongoni mwa shule kongwe 20 nchini ambazo serikali kupitia Wizara ya
Elimu imeweka mpango wa kukarabati shule hizo kwa lengo la kutunza
hadhi na kuziboresha zaidi. Ambapo shule hiyo imepata mgawo wa shilingi
1,123,353,700/=
“Tafadhalini sana Mwalimu Mkuu,
Mkurugenzi, Afisa Elimu na sisi wote tuhakikishe kwamba shule hii
imebadilika kwa kuwa hizi pesa si kidogo, bilioni sio hela kidogo,
zisichezewe, zifanye kazi iliyokususdiwa na kazi yenyewe ioneshe sura ya
bilioni, isijekutokea tukapata kazi nyingine ya kusema kwamba hizi pesa
kazi iliyofanyika ni ya hovyo hovyo,” Mh. Zelote Alisisitiza.
Baada ya kuona juhudi
zinazoendelea katika ukatabati huo Mh. Zelote amesifu uongozi wa shule
wa kuajiri mafundi vijana waliopo mtaani ili kuwa na matumizi mazuri ya
fedha hizo tofauti na kuwatumia wakandarasi ambao wangesababisha fedha
nyingine zipotee bila ya sababu, na kusisitiza kuwa vijana hao
wasimamiwe kwa ukaribu sana na kupewa maelekezo ili wasilipue kazi
inayoendelea.
Pamoja na hayo Mh. Zelote
alilisisitiza uwazi kwenye matumizi ya fedha za umma, na kuwataka
wakaguzi kuwa makini na kukagua kila hatua ya ujenzi na kuona kuwa kila
senti inayotumika inaendana na thamani ya ujenzi inayoonekana
Aidha alizitaka Halmashauri zote
Mkoani Rukwa kutenga bajeti kwa kupitia mapato yake ya ndani ili
kuboresha miundombinu ya shule jambo ambalo linaweza kubadilisha
muonekano wa shule nyingi mkoani humo.
“Ningependa kuona shule hii
inakuwa ya mfano kwakuwa ipo katika makao makuu ya mkoa na pia alishauri
kujenga uzio na kuendeleza utunzaji wa mazingira kwa kuweka sharia kali
kwa wanafunzi ili waendelee kutunza mazingira ya shule,” Mh. Zelote
aliongezea.
Awali alipokuwa akisoma taarifa
fupi ya ukarabati wa shule kongwe Sekondari ya Kantalamba mwalimu Mkuu
wa Shule hiyo Martin Kasansa alitaja changamoto kadhaa zinazorudisha
nyuma kasi ya ukarabati wa shule hiyo ikiwemo uchakavu mkubwa wa bwalo
uliosababisha kuanza upya ujenzi, upatikanaji wa baadhi ya vifaa mkoani
Rukwa kuwa mgumu na kulazimika kuagiza kutoka mkoa wa Mbeya na
kutopatikana kwa maji kumechelewesha ujenzi unaoendelea.
“Kazi ya ukarabati ilianza rasmi
mwezi June 2017 na inasimamiwa na mwandisi kutoka Chuo cha Sayansi na
teknolojia Mbeya na inategemewa kumalika ndani ya miezi mitatu, lakini
upatikanaji wa maji umekuwa ni tatizo katika eneo letu, ” Martin Alisema
Ukarabati unaoendelea katika
shule hiyo unahusisha mabweni 6, vyumba vya madarasa 14, ofisi za
walimu, vyoo, mfumo wa maji safi na maji taka, mfumo wa umeme, jiko,
bwalo, maabara pamoja na jingo la kilimo. Ambapo mapaka sasa Shilingi
648,051,540.90/= imeshatumika na kufikia asilimia Zaidi ya 58.
Nae Katibu Tawala wa Mkoa wa
Rukwa Bernard Makali aliutaka uongozi wa shule kuangalia maeneo muhimu
na kuweaza kuyamalizia ili wanafunzi wasiachwe nyuma na muhula wa mwaka
huu na kusisitiza kuwa upishi wa kutumia kuni si mzuri na kuahidi
kushikiana nao kutafuta namna ya kupikia kwa kutumia gesi jambo ambalo
litatunza mazingira.
No comments:
Post a Comment