Abbas Kondo Gede na Albeto Mandes wamehukumiwa kwenda jela miaka 22 kila moja kwa kosa la kujihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya aina ya Cocaine na Heroin.
Washitakiwa hao ambao walitenda makosa yao kwa nyakati tofauti wamehukumiwa pia kulipa faini ya jumla ya shilingi 320.7 milioni.
Hukumu ya Abbas Kondo Gede ya kwenda jela miaka 22 na kulipa faini ya jumla ya shilingi 175,764,000/= imetolewa leo ( Jumatano) na Mhe. Jaji Korosso baada ya kujiridhisha pasipo shaka kwamba, mshtakiwa alikuwa na hatia ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Abbas Kondo Gede mtanzania, na mkazi wa mtaa wa Lindi, Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam, na ambaye alikuwa ni mcheza mpira wa miguu. Alikamatwa tarehe 14/5/2011 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akitokea Sao Paulo, Brazil, kwa usafiri wa Shirika la Ndege la Quater akiwa na kete 77 sawa na gramu 1,171.75 za cocaine zilizokuwa na thamani ya shilingi 58,588.000/= milioni.
Kesi ya Abbas Gede iliendeshwa na Mawakili wa Serikali Batilda Mushi na Frank Tawala ambapo katika maelezo yao waliiomba Mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.
Kwa upande wa Albeto Mendes ambaye ni raia wa Guinea Besau yeye alikamatwa tarehe 15/4/2012 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa na gram 1,277.41 za Heroine zilizokuwa na thamani ya shilingi milioni 57,483.000/= akiwa katika harakati za kusafiri kwenda nchini Mali.
Hukumu ya Albeto Mendes ya kwenda jela miaka 22 na kulipa faini ya shilingi 144,955,700/= imetolewa leo ( jumatano) na Mhe. Jaji Mfawidhi Matogolo baada ya kujiridhisha pasipo shaka kwamba mshtakiwa alikuwa na hatia.
Mawakili wa Serikali walioendesha kesi hiyo na kuiomba Mahakama kutoa adhabu kali walikuwa ni Joseph Maugo ambaye ni Wakili wa Serikali Mwandamizi na Wakili Clara Chalwe.
Imetolewa na
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Dar es Salaam
20/9/2017
No comments:
Post a Comment