Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Miundombinu Prof. Norman Sigalla King (wa kwanza kushoto) na wajumbe
wengine wa Kamati wakiwa wamekalia mnara wa Halotel wakipata maelezo
kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Halotel Bwana Philemon Joel
(hayupo pichani) kuhusu utayari wa kampuni hiyo kujenga mnara baada ya
mgogoro wa ardhi kumalizika kwenye kijiji kijiji cha Timbolo, kata ya
Sambasha Wilaya ya Arumeru mkoani Manyara
Meneja wa TTCL Mkoa wa Arusha na
Manyara Bwana Brown Japhet (wa pili kushoto) akifafanua jambo mbele ya
wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu (hawapo pichani) ilipofanya
ziara ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini kwenye
kijiji cha Sigino kata ya Singo iliyopo wilaya ya Babati Mjini mkoani
Manyara. Wa kwanza kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa
Wote Eng. Peter Ulanga.
Kaimu Mkurugenzi wa kampuni ya
simu ya Halotel wa Mkoa wa Arusha Bwana Philemon Joel (wa kwanza kulia)
akitoa maelezo kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu (hawapo
pichani) kuhusu utayari wa kampuni hiyo kujenga mnara kwenye kijiji cha
Timbolo, kata ya Sambasha Wilaya ya Arumeru mkoani Manyara baada ya
mgogoro wa ardhi kumalizika. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Idara ya
Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Bwana Albert Richard.
Mwenyekiti wa kijiji cha Timbolo,
kata ya Sambasha wilaya ya Arumeru mkoani Manyara Bwana Samwel Saning’o
akisisitiza umuhimu wa uwepo wa mawasiliano vijijini mbele ya wajumbe wa
Kamati ya Bunge ya Miundombinu wakati wa ziara ya Kamati kwenye kijiji
hicho ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini.
……………………………
Serikali kupitia Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote imeendelea na kazi ya kuhakikisha kuwa wanachi wote
waishio vijijini na maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara wanapata
huduma za mawasiliano kwa wakati ili kuweza kuchangia ukuaji wa uchumi
na upatikanaji wa huduma za kijamii na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Hayo yameelezwa na Mtendajii Mkuu
wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Eng. Peter Ulanga wakati wa
ziara ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu ya kukagua ujenzi wa
minara ya simu za mkononi na upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwenye
maeneo mbalimbali vijijini ya mkoa wa Arusha na Manyara. Eng. Ulanga
amesema kuwa migogoro ya ardhi kwenye baadhi ya vijiji mbalimbali nchini
inachangia ucheleweshaji wa ujenzi wa minara na ufikishaji wa huduma za
mawasiliano vijijini.
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano kupitia Mfuko huu uliweka lengo la kufikisha mawasiliano
kwenye vijiji 4,000 nchi nzima ifikapo mwezi Novemba mwaka huu. Uwepo wa
migogoro ya ardhi unachangia kuchelewesha kampuni za simu zilizopatiwa
ruzuku na Serikali kujenga minara, “mgogoro wa ardhi kwenye kijiji cha
Timbolo kata ya Sambasha Wilayani Arumeru umeichelewesha kampuni ya
Halotel kujenga mnara na hivyo wananchi wa kata hii kukosa mawasiliano
kwa kuwa mgogoro huo umechukua zaidi ya miaka miwili kukamilika
mahakamani,”amesema Eng. Ulanga.
Kaimu Mkurugenzi wa kampuni ya
simu ya Halotel wa Mkoa wa Arusha Bwana Philemon Joel amesema kuwa
mahakama iliweka zuio la ujenzi wa mnara kwenye eneo la kijiji cha
Timbolo kata ya Sambasha ambapo kesi ya mgogoro huo umechukua miaka
miwili kufanyiwa maamuzi kwenye ngazi ya mahakama. “Tumekuwa tukienda
mahakamani mara kwa mara na kupigwa tarehe kuambiwa Hakimu hayupo na
mara nyingine inapita miezi minne bila ya kesi kusikilizwa hivyo
imetuchelewesha kuanza ujenzi,”amesema Bwana Joel.
Naye Mwenyekiti wa kijiji cha
Timbolo, kata ya Sambasha Bwana Samwel Saning’o amesema kuwa Serikali ya
kijiji ilisimama na kusema kuwa wanataka mawasiliano na sio utalii kwa
kuwa kulikuwa na mgogoro baina ya mmiliki wa eneo la jirani na eneo la
mwingine ambapo mnara unatakiwa kujengwa. Bwana Saning’o amemshukuru
sana Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Bwana Alexandra Mnyeti kwa kuingilia kati
mgogoro huu, kusimamia na kuhakikisha kuwa unakamilika ili wananchi
waweze kupata mawasiliano. Eng. Ulanga amesema ujenzi wa mnara wa
Halotel kwenye eneo hili hauwezi kukamilika mwezi Novemba mwaka huu,
hivyo sisi kama Mfuko wa UCSAF tutawapatia muda wa ziada ili waweze
kukamilisha ujenzi wa mnara na wananchi waweze kupata mawasiliano. Pia
Eng. Ulanga amewataka wanachi wa vijiji husika kushirikiana na kampuni
za simu kulinda miundombinu ya mawasiliano na minara ili mawasiliano
yaweze kupatikana muda wote.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Miundombinu Prof. Norman Sigalla King ametoa rai kwa mamlaka
zinazosimamia haki na vyombo vya ulinzi viambata vya Jeshi la Polisi na
mahakama kufanya uchunguzi na kuendesha kesi kwa wakati ili kuharakisha
kutoa haki. “Ukichelewa kutoa shauri la hukumu kwa jambo la umma
linalogusa maslahi ya wananchi unachelewesha maendeleo ya
wananchi,”amesema Prof. Norman Sigalla King. Ameongeza kuwa wananchi
washirikiane na kampuni za simu za mkononi kulinda minara na kutoa ardhi
bila migogoro ili waweze kupata huduma za mawasiliano kwenye vijiji
vyao kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla King ameitaka
Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kukamilisha ujenzi wa minara yake ya
simu kwa wakati kwenye vijiji mbalimbali nchini ili wananchi wa maeneo
husika waweze kupata huduma za mawasiliano. Hayo ameyasema Prof. Norman
Sigalla King wakati wa ziara ya Kamati yake walipotembelea kijiji cha
Sigino kata ya Singo iliyopo wilaya ya Babati Mjini mkoani Manyara.
Naye Meneja wa TTCL Mkoa wa
Arusha na Manyara Bwana Brown Japhet amesema kuwa TTCL imekamilisha
ujenzi wa minara kwenye vituo vyote vya Mkoa wa Arusha na viko hewani
wananchi wanapata mawasiliano. Bwana Japhet ameilieza Kamati kuwa kwa
vituo viwili vilivyobaki vya TTCL kama pale Saitabau, Arusha kulikuwa na
mgogoro wa ardhi ambapo Serikali ya Mkoa imeingilia kati na kumaliza
mgogoro huo na vituo vingine viwili vipo kwenye hifadhi ya Taifa ya
Ngorongoro ambapo vinasubiri tathmini ya mazingira ikamilike ili ujenzi
wa minara kwenye vituo hivyo uweze kuanza na suala hili limefikishwa
Wizara ya Maliasili na Utalii ili liweze kukamilishwa.
Prof. Norman Sigalla King
ameyataka makampuni ya simu kuhakikisha kuwa mawasiliano yanasambaa nchi
nzima. Pia ameitaka TTCL kukamilisha ujenzi wa minara yake kwa wakati
na kuhakikisha kuwa kila wanapopatiwa ruzuku na Serikali wakamilishe
jukumu lao kwa wakati na wafanye kazi kwa ushindani. Ameoneza kuwa
Kamati yake imeridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na TTCL. Kamati
inazitaka mamlaka nyingine zinazohusika na ujenzi wa minara na
upatikanaji wa mawasiliano vijijini washirikiane kwa pamoja na kufanya
maamuzi kwa wakati ili kuwawezesha wananchi kupata huduma za mawasiliano
vijijini kwa wakati.
No comments:
Post a Comment