MAMLAKA ya udhibiti usafiri wa
nchi kavu na majini (SUMATRA),mkoani Pwani ,imewaasa wamiliki wa mabasi
madogo ya abiria(daladala) yanayofanya safari zake Mbezi -Kibaha kuacha
kupandisha nauli tofauti na zilizotangazwa kisheria.
Imesisitiza nauli halali kutoka
mbezi hadi Kibaha ni 500 badala ya 800 wanayoitoza kwa sasa kwa abiria
na Mbezi-Mlandizi ni sh.1,600 badala ya 1,800/2,000 inayolipishwa.
Aidha kuanzia sasa basi litakalobainika kutoza nauli tofauti na elekezi atafikishwa mahakamani ama kutozwa faini.
Hayo aliyasema na ofisa mfawidhi
wa mamlaka ya udhibiti usafiri wa nchi kavu na majini (SUMATRA)mkoani
Pwani, Omary Ayubu,mjini Kibaha baada ya kufanya zoezi la kushtukiza
kukamata magari yenye makosa mbalimbali,kwa kushirikiana na jeshi la
polisi mkoani hapo kupitia kitengo cha usalama barabarani.
Alisema wamekuwa wakipokea malalamiko mengi kutoka kwa abiria kuwa wanatozwa nauli kubwa suala amabalo ni kinyume na sheria.
Ayubu alitaja viwango vya nauli
vinazopaswa kulipwa kuwa ni Mbezi- Kiluvya kwa Komba sh.400 badala ya
sh.700 na Mbezi-Picha ya Ndege sh.700 badala ya 900.
Maeneo mengine ni Mbezi hadi
Mlandizi sh.1,600 badala ya 1,800/2,000, Mbezi- Kongowe sh.1,100,
Mbezi-Vigwaza 2,100, Mbezi-Chalinze 3,200, Mbezi-Lugoba 4,100 na
Mbezi-Msata 4,600 .
“Leo katika operesheni hii tumekamata magari 21 kutokana na makosa ya kutokuwa na ticket na kutoza nauli kubwa “
“Madereva nane watapelekwa
mahakamani kutokana na kuzidisha nauli kinyume cha sheria na tunawataka
wamiliki kuzingatia masharti ya leseni,” alisema Ayubu.
Alisema wataendelea kuwachukulia
hatua za kisheria madereva wanaokiuka sheria na ameshukuru wananchi kwa
ushirikiano wao wa kutoa taarifa juu ya magari yanayoendelea kutoza
nauli ambazo ni kinyume cha utaratibu.
Ayubu aliwataka madereva kuwa na
katabia ka kugomo kwani haina faida na badala yake mwenye malalamiko
aende ofisini na kuandika barua ndani ya mwezi mmoja ili malalamiko yao
yaweze kutafutiwa ufumbuzi.
Nae kamanda wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Pwani,Salum
Morimori alisema kuwa walifanya ukaguzi kwenye mabasi hayo ili kuangalia
ubora wa magari .
Alieleza kumekuwa na malalamiko
toka kwa abiria kutopewa tiketi, abiria kuchanganywa na mizigo ,ubovu wa
magari,matairi mabovu na kuchakaa kwa viti kwenye magari hayo.
Morimori alisema ,hadi sasa magari
35 yamekamatwa ,kati yake 21 ni makosa yanayosimamiwa na SUMATRA na 14
ni ya kiusalama barabarani.
“Tumefanya zoezi hili la
kusthtukiza kwa kushirikiana na wenzetu SUMATRA ili kuwajengea
kumbukumbu madereva kufuata sheria za usalama barabarani,” alisema
Morimori.
Hata hivyo, alisema kuwa lengo ni kuhakikisha usalama wa wanajamii hasa wanaotumia vyombo vya moto wabaki salama.
“Wamiliki na madereva wahakikishe
wanaboresha vyombo vyao viko salama kwa kufanya marekebisho hasa mipira
na tunahitaji wanajamii kushirikiana nasi ili kukabiliana na madereva
ambao wanakiuka sheria za usalama barabarani” alisema Morimori.
No comments:
Post a Comment