KATIBU Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. Doto James amewatoa hofu watanzania kuhusu ongezeko la Deni
la Taifa akisisitiza kuwa Deni hilo ni himilivu.
Bw. James amesema hayo Jijini Dar
es Salaam kwa vyombo vya habari wakati wa hafla fupi ya kutia saini
Mkataba wa mkopo wenye masharti nafuu wa Shilingi bilioni 340 uliotolewa
na Benki ya Dunia kwa ajili ya Mradi wa kuendeleza utalii kwa vivutio
vilivyoko katika ukanda wa kusini mwa Tanzania ujulikao kama Resilient
Natural Resource for Tourism and Growth (REGROW)
Alikuwa akitolea ufafanuzi kuhusu
baadhi ya watu na vyombo vya habari vinavyozungumzia Deni la Taifa kwa
kutumia neno Deni la Taifa “linapaa”
Katibu Mkuu huyo ambaye pia ndiye
Mlipaji Mkuu wa Serikali alisema kuwa Deni la Taifa ni himilivu kwa
kutumia viwango vya kitaifa na kimataifa kwamba ili nchi iwe katika
hatari ya kukua kwa Deni lake la Taifa inabidi lifikie asilimia zaidi ya
50 lakini kwa Tanzania kiwango cha deni hilo ni asilimia 32.
“Deni letu lingekuwa linapaa, hata
Benki ya Dunia wasingekubali kutukopesha kwa maana hiyo tukitaka kukopa
tutafanya hivyo kwa kuwa tuko chini katika viwango vya ukopaji kwa
asilimia zaidi ya 18” alisema Bw. Doto James.
Kwa hiyo nawaomba hili mlichukue muuelimishe umma wa watanzania kwamba deni la Taifa ni stahimilivu, nchi inakopesheka vizuri.
Novemba 7, 2017, Waziri wa Fedha
na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiwasilisha Bungeni mjini
Dodoma Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa
Maanndalizi ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2018/2019 alisema kuwa Deni la
Taifa limefikia dola za Marekani milioni 26,115.2 mwezi Juni mwaka
2017.
Dkt. Mpango alieleza kuwa ongezeko
hilo ni sawa na asilimia 17 ikilinganishwa na dola milioni 22,320.76
katika kipindi kama hicho mwaka 2016.
Alisema ongezeko hilo lilichangiwa na mikopo mipya iliyochukuliwa ili kugharamia miradi ya maendeleo kama vile: Standard Gauge Railway; Strategic Cities; mradi wa usafirishaji Dar es Salaam (DART) na kupanua upatikanaji wa maji safi Dar es Salaam.
Deni hilo la Taifa linajumuisha
deni la Serikali lililofikia dola za Marekani milioni 22,443.70 na deni
la sekta binafsi la dola za Marekani milioni 3,671.50. Pamoja na
ongezeko hili, viashiria vyote bado vinaonesha kuwa deni la Taifa ni
himilivu kwa kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu huku uwiano kati
ya deni na Pato la Taifa umefikia asilimia 31.2 ikilinganishwa na ukomo
wa asilimia 56.
No comments:
Post a Comment