Kaimu Katibu Tawala Sehemu ya
Maji Mkoa wa Singida Mhandisi Lyidia Joseph amebainisha hayo leo wakati
wa kikao maalumu na Timu ya usimamizi wa sekta ya maji ya halmashauri ya
Wilaya ya Manyoni, kwa ajili ya kufuatilia usimamizi na utekelezaji wa
miradi ya maji.
Mhandisi Lydia amewaeleza
wataalamu hao kuwa uongozi wa mkoa hautavumilia endapo kuna mtumishi
yeyote atafanya mzaha katika kusimamia miradi ya maji kwakuwa mkoa
umekuwa ukitoa ushirikiano wa kutosha hivyo hakuna sababu ya kushindwa
kufanya vizuri.
“Sisi katika ngazi ya mkoa
hatutavumilia mzaha katika masuala ya maji, tupo tayari kutoa
ushirikiano popote mnapoona mnakwama ili tu tufikie malengo yetu ya
kutoa huduma bora za maji kwa wananchi, hali ilivyo sasa hairidhishi
kabisa, tufanye kazi kwa kasi zaidi”, ameongeza Mhandisi Lydia.
Amesema, halmashauri hiyo
inapaswa kuhakikisha inatekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt
Rehema Nchimbi la kuongeza asilimia ya upatikanaji wa maji katika
halmashauri hiyo kutoka 45 hadi 72 ifikapo mwezi Juni, 2018 pamoja na
kuandaa takwimu sahihi za upatikanaji wa maji ifikapo Disemba mwaka huu.
Mhandisi Lydia amefafanua kuwa
halmashauri hiyo itaweza kuongeza asilimia ya upatikanaji maji na
kufikia lengo la asilimia 72 endapo watendaji wote hasa wajumbe wa timu
ya usimamizi wa sekkta ya maji, watashirikiana kusimamia ujenzi wa
miradi mitano pamoja na ukarabati wa miradi minne iliyopo kwenye bajeti.
“Kila Mjumbe hapa ana kazi ya
kufanya katika miradi hii ya Makanda, Nyaranga, Kikombo, Makutopola na
Kicheho inayojengwa pamoja na ile ya Sanza, Mkwese, Londoni na Sorya
inayokarabatiwa, Kitengo cha ugavi kisimamie taratibu za manunuzi
zinafuatwa pamoja na kuhakiki ubora wa mkandarasi, mwanasheria aelekeze
taratibu za kisheria, Maendeleo ya jamii ahakikishe wananchi wanaujua
mradi vizuri, kila mmoja akitekeleza jukumu lake ipasavyo tutafikia
lengo”, ameeleza na kuongeza kuwa,
“Idara ya maji msifanye siri
miradi ya maji na kujifungia wenyewe hakikisheni timu hii ya usimamizi
wa sekta yenu inafahamu vizuri miradi yote ya maji pamoja na kusimamia
utekelezaji wa miradi hiyo, mkifanya hivyo mtaenda kwa kasi na kazi
itafanyika kwa ufanisi, sio kila kitu mfanye wenyewe tu”, ameongeza
Mhandisi Lydia.
Aidha Mhandisi Lydia amempongeza
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Charles Fussi kwa kujitoa
kwake katika kusimamia na kutoa fedha za kusaidia miradi ya maji akitoa
mfano wa kiasi cha milioni 16 zilizotolewa na mkurugenzi huyo kutoka
katika makusanyo ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji.
Naye Mhandisi wa Maji kutoka
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Athanas Nziku ameieleza timu hiyo kuwa usimamizi
wa jumuiya za watumia maji ni jambo muhimu kwakuwa takwimu zimeonyesha
jumuiya hizo zimekuwa zikikusanya pesa nyingi sambamba na matumizi
makubwa ya fedha wanazokusanya.
Mhandisi Nziku amewafafanulia
kuwa jumuiya hizo za watumia maji zinapokusanya fedha nyingi sambamba na
kutumia fedha nyingi ni moja ya kiashiria kuwa miradi hiyo ya maji
inaweza kufa hivyo wazitembelee na kuona tatizo liko wapi endapo liko
ndani ya uwezo wa halmashauri liweze kutatuliwa mapema.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya
Mkwese na Mwenyekiti wa huduma za Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya
Manyoni Robert Kenze amesema, halmashauri hiyo imedhamiria kuboresha
huduma za maji ambapo ajenda ya maji imewekwa kipaumbele katika vikao
vyote muhimu.
Kenze amesema wakuu wa Idara wa
halmashauri hiyo watashirikiana na Idara ya maji wilayani humo huku
wanasiasa wakiwa tayari kutoa elimu na kusimamia utekelezaji wa miradi
ya maji.
No comments:
Post a Comment