Yanga ilifungwa kwa mikwaju ya penalti 4-1 katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu bara walikuwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyopatikana kipindi cha kwanza kupitia kwa mshambuliaji wao Donald Ngoma kabla Azam haijasawazisha mabao hayo katika dakika ya 75 na 90 yaliyofungwa na John Bocco na Shomari Kapombe na hivyo mechi hiyo kwenda kwenye kupigiana mikwaju ya penalti.
Akizungumza na gazeti hili jana Pluijm alisema kupoteza taji hilo haimaanishi kwamba watashindwa kutetea mataji yao mengine. Yanga inashikilia taji la Ligi Kuu na lile la Kombe la Shirikisho la TFF (FA).
“Mechi ya jana (juzi) ushindani ulikuwa mkali sana, wenzetu walituzidi kwenye penalti wakatufunga, lakini timu yangu pia haikucheza vibaya,” alisema. “Lakini wachezaji wangu hawajapumzika vya kutosha kama ilivyo wa timu nyingine kutokana na kushiriki kwenye mashindano, hilo nalo pia limechangia maana ni wachovu,” alisema.
Yanga ipo hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na keshokutwa inatarajiwa kukamilisha ratiba kwa kumenyana na TP Mazembe ya Congo DR mjini Lubumbashi.
“Lakini kufungwa na Azam sio kwamba tutashindwa kutetea mataji yetu mengine, timu yangu bado nzuri na nina uhakika wa kufanya vizuri kwenye kutetea mataji tunayoyashikilia,” alisema Pluijm.
Aidha alisema ataitumia mechi na Mazembe kufanya maandalizi yake ya mwisho kabla ya kuanza mechi za ligi.
Yanga itaanza mechi yake ya kwanza ya kutetea taji la Ligi Kuu Agosti 27 ambapo itacheza na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
“Tukirudi tutajua namna ya kufanya na makosa yaliyotokea kwenye mechi ya Azam tutayafanyia kazi na Mazembe,” alisema.
No comments:
Post a Comment