MFANYABIASHARA maarufu na Mmiliki wa Shule ya Sekondari Merinyo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, Roman Shirima (74), aliyejiua kwa kujilipua, atazikwa kesho Rombo.
Tukio hilo limevuta hisia kali za wakazi wa Moshi na viunga vyake huku simanzi na vilio vya waombolezaji, vikitanda nyumbani kwa marehemu. Mmoja wa majirani wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina moja la Shirima, alisema katika uhai wake, Roman Shirima alijitahidi mno kuwekeza katika shule yake hiyo.
Alisema sekondari hiyo ya Merinyo ni ya bweni na hadi sasa wameshahitimu wanafunzi wa kidato cha nne mara tatu tangu ilipoanzishwa. Shirima alisema kwa sasa wanajiandaa na maziko yatakayofanyika kesho wilayani Rombo.
Alieleza kuwa kama ilivyo desturi yao, tayari kila kaya imekwishachanga Sh 5,000 kwa ajili ya msiba huo. Majirani wengine walisema hadi sasa imekuwa vigumu kuamini tukio hilo, kutokana na mahusiano mazuri, aliyokuwa nayo mzee huyo na majirani.
Walisema tukio hilo limewaacha midomo wazi kutokana na maamuzi magumu, yaliyofanywa na mwenzao, ambaye alikuwa mstari wa mbele kanisani (mzee wa dini) na alikuwa anaketi kiti cha mbele katika ibada.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa alisema tukio la mfanyabiashara huyo kujiua lilitokea Agosti 18 saa 11:25 alfajiri nyumbani kwake eneo la Mjohoroni kata ya Msaranga Ng’ambo iliyopo Manispaa ya Moshi.
Kamanda Mutafungwa alisema siku ya tukio, mfanyabiashara huyo alichukua mafuta ya petroli na kujimwagia mwili mzima katika shamba lake la mahindi, lililopo uani mwa nyumba yake, kisha kujiwasha na kiberiti, hali iliyomfanya aungue vibaya na kusababisha kifo chake papo hapo.
Alisema chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana na kwamba jeshi hilo bado linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha mfanyabiashara huyo kujiua mwenyewe. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi kusubiri taratibu za maziko.
No comments:
Post a Comment