KOCHA Mkuu wa JKT Ruvu, Malale Hamsini amesema kikosi chake kipo tayari kuanza Ligi Kuu Tanzania bara kwa ushindi katika mchezo dhidi ya Simba utakaochezwa mwishoni mwa wiki hii.
JKT Ruvu ilikuwa ianze mchezo wa kwanza dhidi ya Yanga wiki iliyopita lakini mechi hiyo iliahirishwa ili kuipa nafasi Yanga ijiandae na mechi ya kimataifa ya kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe ya Congo DR na hivyo Ruvu kulazimika kusubiri mechi dhidi ya Simba.
Kocha Hamsini aliliambia gazeti hili wachezaji wako imara tayari kwa mchezo huo utakaochezwa Taifa lakini JKT akiwa ni mwenyeji.
“Wachezaji wote wako vizuri na tunatarajia kupambana mwanzo mwisho kupata ushindi wa kwanza ambao utatusaidia kujua tunakwenda wapi,” alisema.
Mchezo huo utakuwa mtihani wa kwanza kwa Hamsini kama kocha wa timu hiyo baada ya kukabidhiwa mikoba ya Abdallah Kibadeni ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa ufundi wa timu hiyo. Hamsini ana wasaidizi wapya ambao ni wachezaji waliostaafu katika kikosi hicho George Minja na Amos Mgisa.
Nahodha wa timu hiyo Michael Aidan alisema ushindi katika mchezo huo ni lazima kwani wachezaji wamefanya mazoezi ya muda mrefu na kuonesha morali ya kutaka kupambana kwa ajili ya kupata pointi tatu. Simba imeanza vizuri ligi baada ya kuifunga Ndanda mabao 3-1 katika mechi yake ya ufunguzi na imepania kupata ushindi pia kwa timu zote zinazofuata
No comments:
Post a Comment