YANGA jana imeaga rasmi michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufungwa mabao 3-1 na TP Mazembe ya Congo DR katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Stade TP Mazembe mjini Lubumbashi.
Habari kutoka Lubumbashi zinasema katika mechi hiyo ya hatua ya makundi, Mazembe ilipata bao la kuongoza dakika ya 28 likifungwa na J Bolingi.
Aidha Yanga ilimaliza mechi hiyo pungufu baada ya beki wake Vicent Andrew kutolewa kwa kadi nyekundu katika dakika ya 30 baada ya kufanya madhambi.
Bao la pili la Mazembe lilifungwa dakika ya 55 na Rainford Kalaba baada ya kupigwa shuti kali lililopanguliwa na kipa wa Yanga Deogratius Munishi na kumkuta mfungaji huyo aliyemalizia kwa urahisi. Bao la tatu lilifungwa dakika ya 64 na Bolingi.
Yanga ilipata bao la kufutia machozi dakika ya 74 baada ya mpira wa adhabu aliopiga Haruna Niyonzima kugonga mwamba wa juu kisha Amiss Tambwe akaumalizia wavuni.
Licha ya Yanga kufanya mabadiliko katika kikosi chake ya kumtoa Simon Msuva na kumwingiza Juma Mahadhi, bado hayasaidia kuikoa timu hiyo iliyotamani kumaliza mchezo kwa kuweka rekodi ya kufunga.
Yanga iliyofika hatua hiyo kwa mara ya kwanza baada ya mwaka 1998 ilipocheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, imeaga michuano hiyo ikiwa imeshinda mechi moja kati ya mechi sita ilizocheza.
Iliifunga Mo Bejai bao 1-0, ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Medeama kwenye uwanja wa nyumbani, ikifungwa bao 1-0 nyumbani dhidi ya TP Mazembe, ikafungwa bao 1-0 na Mo Bejaia mabao 3-0 kabla ya jana kumaliza na Mazembe ugenini.
Kwa matokeo hayo, Yanga imemaliza michuano hiyo mkiani mwa kundi A ikiwa na pointi nne, kundi hilo linaongozwa na TP Mazembe yenye pointi 13 ikifuatiwa na Medeama yenye pointi 8 na Mo Bejaia yenye pointi tano.
Medeama na Bejaia zilitarajiwa kucheza jana jioni. Timu mbili za juu kutoka kila kundi zinafuzu nusu fainali.
Hata hivyo timu hiyo bado itaendelea kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa mwakani kwani ndio bingwa wa ligi msimu uliopita hivyo itashiriki tena michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika
No comments:
Post a Comment