Aidha, timu ngeni Mbao FC, Majimaji, Stand United na Toto Africans zimetabiriwa kushuka daraja katika msimu huu kama hazitajizatiti kutokana na maandalizi ya kulipua.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti jana, baadhi ya wachambuzi wa soka, wachezaji wa zamani na makocha walisema Yanga, Simba na Azam zitakuwa bora kutokana na maandalizi na usajili walioufanya ukilinganisha na timu nyingine.
Miongoni mwa wachambuzi hao ni Ally Mayay aliyewahi kucheza Yanga na timu ya taifa alisema kuwa timu za Azam, Simba na Yanga zitaendelea kuwa tishio na zenye ushindani mkali msimu huu.
Akitolea ufafanuzi kuhusu Simba kuwa itakuwa bora msimu huu ukilinganisha na msimu uliopita kutokana na kusajili wachezaji wazuri akiwemo Mrundi, Laudit Mavugo na wengine kadhaa.
“Simba msimu huu wanaonekana watakuwa wazuri na kuleta ushindani kwa timu ambazo zilikuwa shindani katika kipindi cha misimu karibu minne mfululizo kwa maana ya Azam na Yanga, nimeangalia usajili wake na maandalizi ni mzuri,”alisema.
Mayai alisema pia, Simba itakuwa na ushindani kutokana na kuingia katika mfumo mpya wa Kampuni ambao utatoa fursa kwa mmoja wa wanachama wao Mohamed Dewji ‘Mo’ kumwaga fedha na kuwa na bajeti nzuri ya maandalizi.
Alisema ukilinganisha na msimu uliopita Simba ilishindwa kufanya vizuri kwa kuwa haikuwa na bajeti nzuri iliyokuwa ikifanana na Yanga na Azam lakini sasa wamepata mtu ambaye atawapeleka huko na kuleta ushindani katika ligi.
Mchezaji huyo wa zamani wa Yanga alisema timu zitakazoendelea kutikisa nafasi ya katikati ni Mtibwa Sugar, Mwadui, Prisons na Ruvu Shooting.
Pia, alisema timu za Toto Aficans, Mbao FC, Majimaji, JKT Ruvu na Ndanda FC bado zitakuwa chini kutokana na maandalizi yake kuwa madogo na hata usajili wao haukueleweka vizuri huku akisema Stand United haieleweki kutokana na mgogoro unaoendelea.
Naye Kocha Msaidizi wa Simba, Jakson Mayanja alisema anafikiri timu zote 16 zitakuwa ngumu na zenye ushindani. Alisema sababu ni kwa vile kwa uzoefu wake anaona wakati mwingine unaweza kufikiri timu fulani itakuwa nzuri lakini baadaye ikaanza kufanya vibaya kutokana na ushindani.
Mayanja alisema kila timu inaonekana kujiandaa vizuri kutokana na usajili wake na maandalizi yake. Kwa upande wa Kocha wa Mwadui FC, Jamhuri Kihwelu alisema timu zote nzuri lakini anafikiri Azam italeta ushindi mkubwa kutokana na kuwa na makocha wapya na kusajili wachezaji wazuri.
Alisema kwa kuangalia mchezo wake wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga juzi, anafikiri itakuwa timu bora ukilinganisha na Yanga licha ya kuwa ni nzuri na yenye ushindani imechoka kutokana na kutopata muda wa kupumzika kufuatia mfululizo wa michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Pia, alisema kwa upande wa Simba italeta ushindani vile vile kwa kuwa imesajili wachezaji wazuri.
“Timu zote ni nzuri na zimesajili vizuri. Lakini ukweli Azam FC ni timu ambayo naona itakuja na ushindani msimu huu. Yanga imecheza mashindano mengi imechoka lakini bado iko vizuri na hata kwa Simba pia,” alisema.
No comments:
Post a Comment