WAKUU wa mikoa, wilaya na watendaji wa mamlaka wa serikali za mitaa, wametakiwa kusimamia mipango ya kibajeti katika halmashauri ili bajeti hizo zilenge kutatua matatizo ya wananchi wao.
Agizo hilo, lilitolewa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene, wakati akifungua kikao cha kazi kwa wakuu wa mikoa, makatibu tawala, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa mamlaka wa serikali za mitaa wa mikoa ya Dodoma, Pwani, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara na Morogoro.
Waziri Simbachawene alisema, wakuu wa mikoa na wilaya wanao wajibu wa kushiriki katika mipango ya kibajeti ya halmashauri ili kuona kuwa bajeti zinazoandaliwa zinalenga kuwasaidia wananchi.
Alisema ushirikishwaji wa wananchi katika mipango hiyo ya bajeti ni muhimu ili waweze kuibua fursa na vikwazo vinavyojitokeza katika kufanya maendeleo yao.
Simbachawene alitumia fursa hiyo kuwasilisha pongezi zilizotolewa kwa nyakati tofauti wa viongozi wakuu wa Serikali akiwamo Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kuhusu utendaji mzuri wa wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa , wakuu wa wilaya na wakurugenzi watendaji wa halmashauri hizo.
Hivyo aliwataka wateuliwa hao kutekeleza majukumu yao kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu ili kusiwe na mwingiliano wa majukumu ya kikazi katika kuendelea kuboresha utendaji wao.
Alisema bado makusanyo ya mapato katika halmashauri nyingi hayaridhishi kutokana na kushindwa kufikia asilimia 10 hali inayoifanya Serikali Kuu kuendelea kutoa ruzuku kwa ajili shughuli za maendeleo na za kiutendaji.
Waziri Simbachawene pia aliwasihi wakurugenzi wa halmashauri kutokubali kuingiliwa na nguvu za kisiasa katika utendaji kazi ili kuepuka kuingiliana na madiwani wanaolazimisha kampuni zao kupata zabuni za makusanyo ya halmashauri na hatimaye kushindwa kusimamia makusanyo hayo.
Waziri Simbachawene aliwashauri wakuu wa mikoa na wilaya kufuatilia taarifa za mikutano mikuu ya vijiji ili kujua maazimio yao na kuona namna ya kutatua changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na kuona taarifa za mapato na matumizi zinazomwa kwenye mikutano ya kijiji kulingana na sheria za serikali za vijiji.
Awali, akimkaribisha Waziri Simbachawene, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe, alitumia fursa hiyo kuwahamasisha viongozi waliohudhuria kikao hicho kuwekeza katika makazi na masuala ya kiuchumi mkoani humo.
Akimshukuru Waziri Simbachawene kwa niaba ya washiriki wenzake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, aliahidi kutozifumbia macho changamoto watazokutana nazo katika utendaji wao katika halmashauri zilizopo kwenye mikoa yao
No comments:
Post a Comment