TIMU ya taifa ya Tanzania Bara ya wanawake, Kilimanjaro Queens, iliyotwaa taji la michuano ya kwanza ya Afrika Mashariki na Kati ya Cecafa ilitua jijini Dar es Salaam jana na kupokewa kishujaa.
Kilimanjaro Queens ilitua kwenye Uwanja wa Kimataifa wa ndege wa Julis Nyerere (JNIA) saa 12:05 jioni badala ya saa 7 mchana kama ilivyotangazwa awali, ililakiwa na wadau mbalimbali wa soka wakiwemo mashabiki wa Taifa Stars.
Mashabiki hao walifika uwanjani hapo kabla ya saa saba mchana wakifuata ratiba ya awali lakini na hata pale ilipobadilishwa, waliendelea kukaa uwanjani hapo wakisubiri timu hiyo.
Awali kabla ya kupanda ndege jijini Mwanza, Mkuu wa Mkoa huo, John Mongela aliipongeza na kuwapa zawadi ya Sh milioni 1 kwa ushindi huo baada ya kuifunga 2-1 Kenya katika fainali huko Jinja, Uganda.
Mongela ameiomba timu hiyo ihakikishe inafanya juhudi kuendelea kuwa mabingwa.
Mwenyekiti wa Soka la Wanawake nchini(TWFA) Amina Karuma ameomba kampuni ziendelee kujitokeza katika kudhamini soka la wanawake.
Karuma pia amepongeza Kampuni ya Airtel na Azam kwa juhudi zao za kusaidia timu hiyo wakati ilipokuwa Uganda.
Karuma alisema ushindi huo umetokana na matunda ya michuano ya Airtel Rising Star, ambapo wameweza kupata wachezaji. Kwa upande wake Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sebastian Mkomwa alisema michuano hiyo ilikuwa migumu sana kwa kuwa walihofia timu za Kenya na Ethiopia kutokana na kucheza michuano ya Afcon kwa wanawake.
Aliomba wachezaji wawe wanaingia kambini mapema sana ili kujianda mapema katika mashindano yoyote yale.
Nahodha wa timu hiyo, Sophia Mwasikili ameiomba serikali iwekeze zaidi katika soka la wanawake hiyo itasaidia kufanya vizuri zaidi. Mwasikili alisisitiza wachezaji wawe wanajaliwa zaidi katika posho zao na mishahara kwa wakati hiyo italeta motisha na kuwawezesha kufanya vizuri.
No comments:
Post a Comment