NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura atakuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Msanii yatakayofanyika Oktoba 29 katika kijiji cha Makumbusho Kijitonyama.
Katika maadhimisho hayo ya kilele, wasanii mbalimbali watapewa tuzo katika kutambua, kuhamasisha na kuthamini mchango mkubwa wanaoutoa hapa nchini.
Mratibu wa siku hiyo ya Msanii, Godfrey Mahendeka alisema kuwa pia siku hiyo kutakuwa na burudani kabambe kutoka kwa wasanii mbalimbali, baadhi yao wakiwa Juma Nature, Peter Msechu na Misoji katika Bongo fleva.
Kwa upande wa muziki wa dansi kutakuwa na kundi la Chamudata All Stars, ambalo litaundwa na wasanii maarufu wa zamani watakaoungana kutoa burudani pamoja.
Alisema kundi lingine la muziki wa dansi litakalotumbuiza ni lile la Ifakara Band na John Kitime. Pia kutakuwa na muziki unaopendwa sana na vijana sasa wa Singeli, ambao utaongozwa na kundi la Hamsha pamoja na makundi mengine.
Ngoma za asili nazo zitakuwepo likiwemo kundi la Mandela, Safari Group na sarakasi wakati kwa upande wa taarab litakuwepo kundi la Siza Segere na lile la Super Shine lenye maskani yake Magomeni jijini Dar es Salaam.
Alisema mchekeshaji Mlugaluga na wachekeshaji mbalimbali watakuwepo huku Ma DJ kama akina Ibony Moalim, John Pantalikis watakuwepo pamoja na dansa wa zamani Athuman Digadiga. Pia kutakuwa na burudani kabambe ya nyimbo za Injili kutoka kwa waimbaji mahiri, ambao mbali na kutoa burudani pia wataiombea amani ya Tanzania.
Siku ya Msanii ni mradi uliobuniwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) ukiwa na lengo la kutambua, kuthamini na kuhamasisha kazi na mchango wa wasanii hapa nchini.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni Nguvu ya Sanaa, ambapo tayari uzinduzi wake ulishafanyika tangu Mei 26 mwaka huu na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye aliwakilishwa na Katibu wake Profesa Elisante ole Daniel.
No comments:
Post a Comment