MAJESHI nchini yamepewa mwito yashirikiane kwa kuweka nguvu kazi ya pamoja kutafuta maeneo ya kujenga nyumba kwa ajili ya kutatua changamoto ya uhaba wa nyumba kwa maofisa wa majeshi hayo.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alitoa mwito huo mjini Shinyanga alipokutana na watumishi wa taasisi mbalimbali za jeshi zikiwemo Polisi, Uhamiaji, Magereza na Zimamoto.
Alisema taasisi za majeshi nchini hasa Polisi zina uhaba wa nyumba, hivyo kuhitaji nguvu ya pamoja. Alisema kwa kushirikiana, inawezekana ikafikia wakati watumishi wa taasisi hizo wakaacha kuishi uraiani kwa sababu ya kuwa na nyumba za kutosha za taasisi zao.
“Kwa umoja wetu tupate maeneo ya kujenga tuwatumie wenzetu wa jeshi la magereza wenye nguvu kazi na kutafuta wafungwa wenye uwezo wa kufyatua matofali ili watufanyie tathmini kuwa ni matofali mangapi yanahitajika ili kuweza kujenga nyumba za kutosha na zenye ubora,” alisema Mwigulu.
Alisema kwa kuungana, kazi hiyo inaweza kufanyika kwa miezi mitatu.
Mwigulu alisema kwa tathmini ya haraka katika makusanyo ya mwezi kwa Polisi nchi nzima hufikia Sh bilioni nne ambapo kwa miaka minne fedha hizo zinaweza kujenga nyumba zote za Polisi bila kukopa kwenye taasisi za fedha. Aidha, alisema masuala hayo ni utekelezaji wa agizo la Rais na alisema mikoa itakayoanza mapema itakuwa ya mfano.
No comments:
Post a Comment