NDEGE ya moja kati ya mbili zilizonunuliwa na Serikali kuimarisha usafiri wa anga nchini, inatarajiwa kuwasili nchini Jumanne ijayo.
Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema leo bungeni mjini Dodoma wakati anatoa taarifa ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa.
Dk Ackson amesema, Waziri Mbarawa amemuarifu kuwa, ndege hiyo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Ametoa mwito kwa wabunge na viongozi kushiriki kuipokea ndege hiyo aina ya Dash 8-Q400 yenye uwezo wa kubeba abiria 76.
Leo wakati anahitimisha vikao vya Bunge vya Mkutano wa Nne wa Bunge la 11, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amelieleza Bunge kuhusu mikakati ya Serikali katika kuimarisha usafiri wa anga kuanzia mwaka huu wa fedha.
Amesema, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, imedhamiria kurejesha fahari ya sekta hiyo nchini kwa kuchukua hatua kadhaa, ikiwamo ya kununua ndege na kuboresha viwanja vya ndege nchini, akisisitiza kuwa, lengo ni kuhakikisha kuwa kila mkoa unakuwa na kiwanja cha ndege cha kisasa, chenye ubora unaofaa kutua ndege.
"Taratibu za kununua ndege nyingine mbili zenye ukubwa wa kati zitakazokuwa na uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 110 zimeanza. Ndege hizo zitahudumia soko la kikanda,” amesema Waziri Mkuu.
Amesema, Serikali pia imeanza kazi ya kuiunda upya ATCL, baada ya Rais kufanya uteuzi wa Mtendaji Mkuu mpya wa ATCL, Ladislaus Matindi na pia Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, Emmanuel Korosso.
No comments:
Post a Comment