• Breaking News

    ..

    ..

    Friday, 16 September 2016

    UKUTA Waiponza Redio ya Lowassa....Yafungwa Kwa Miezi 3 na Faini



    Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia Kamati yake ya Maudhui imekifungia kituo cha Redio 5 Arusha kwa kipindi cha miezi mitatu pamoja na kukitoza faini ya sh. Milioni 5 kwa kosa la kukiuka baadhi ya Kanuni za Huduma za Utangazaji (maudhui) kupitia kipindi chake cha Matukio kilichorushwa Agosti 25, 2016.

    Kwa mujibu wa taarifa ya kamati hiyo, katika kipindi hicho Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Mh. Godbless Lema alitamka maneno ya kashfa yaliyolenga kumdhslilisha Rais John Magufuli na serikali kwa ujumla.

    Wakati akisoma maamuzi ya kamati hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui Joseph Mapunda, aliongeza kuwa kituo hicho pia kilirusha maneno yaliyo tamkwa na Lema ambayo yalikuwa yakihamasisha wananchi kushiriki katika maandamano ya Ukutayaliyopigwa marufuku na Jeshi la Polisi.

    “Maneno ya Lema yalilenga kuhamasisha wananchi kupambana na jeshi la polisi na hivyo kusababisha uvunjifu wa amani na kuhatarisha usalama wa Taifa,” alisema.

    Mapunda alisema uamuzi huo umetolewa na kamati hiyo baada ya kamati hiyo kusikiliza maelezo ya utetezi yaliyotolewa na wa Uongozi wa Redio 5 Arusha.

    “Baada ya kusikiliza maelezo ya utetezi kamati imeridhia kuwa kipindi cha matukio kilikiuka baadhi ya kanuni za maudhui namba 5(a,b,c,d,f,h) 6(2) (b, c) na 18 (1) (b),” alisema.

    Aliongeza kuwa ” kituo hicho kinatozwa faini ya sh. Milioni 5 ambazo zitatakiwa kulipwa ndani ya siku 30 kuanzia leo, kinafungiwa kwa miezi 3 na kuwekwa chini ya uangalizi maalumu kwa muda wa Mwaka 1 baada ya kipindi cha kufungiwa kumalizika, “

    Hata hivyo, Mapunda alisema haki ya wahusika kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo iko wazi ndani ya siku 30 kuanzia leo.

    Kwa upande wa kituo cha redio cha Magic Fm ambacho nacho pia kwa mujibu wa kamati hiyo kinadaiwa kukiuka kanuni za maudhui kupitia kipindi chake cha Morning Magic kipengele cha Paka Rangi ambapo kilirusha maneno yanayodaiwa kumkejeli rais na wananchi, kimepewa onyo kali pamoja na kutakiwa kuomba radhi kwa muda wa siku tatu mfululizo.

    “Baada ya kusikiliza na kutafakari kwa kina maelezo ya utetezi yaliyotolewa na Uongozi wa Magic Fm Redio, Kamati ya Maudhui imeridhika kuwa kipindi cha Morning Magic kilikiuka baadhi ya kanuni za huduma za utangazaji 2005. Kamati ya maudhui inaamua kutoa onyo kali kwa Magic Radio, ” alisema na kuongeza.

    “Pia inatakiwa kumuomba radhi Rais John Magufuli, wasikilizaji na wananchi kwa ujumla. Tangazo la kuomba radhi litolewe kwa siku tatu mfululizo katika taarifa za habari za saa 10.00 alasriri, na 3.00 usiku kuanzia tarehe 17,9,2016.”

    No comments:

    Post a Comment

    HABARI

    HABARI

    MICHEZO

    LOGO

    LOGO

    MAOJIANO

    BURUDANI