WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ameiagiza Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (BCEG) inayofanya ujenzi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza kuhakikisha inakamilisha kazi ndani ya miezi sita ijayo.
Akizungumza baada ya kufanya ukaguzi wa uwanja huo jana katika kuhakikisha agizo la Rais John Magufuli alilolitoa hivi karibuni jijini Mwanza mkandarasi kuendelea na ujenzi huo baada ya kusitisha kwa kukosa pesa, Profesa Mbarawa alisema kazi hiyo inaweza kukamilika kwa haraka iwapo wasimamizi watafanya kazi kwa uadilifu.
“Mkandarasi mshauri unatakiwa kuhakikisha unasimamia kazi kwa uadilifu, kikubwa ni kutopeleka madai yasiyo ya kweli huku serikali ikijipanga kulipa deni lote ili uwanja huo uweze kukamilika ndani ya miezi sita ijayo,” alisema Profesa Mbarawa.
Profesa Mbarawa aliyekagua uwanja huo pamoja na barabara ya Furahisha yenye urefu wa kilometa tano akitokea mkoani Kagera kuangalia madhara yaliyotokana na tetemeko la ardhi, alisema, kazi kubwa zilizobaki katika uwanja huo kwa sasa ni umaliziaji wa jengo na kuweka zege.
Alisema licha ya kazi hizo ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi na mkandarasi, nyingine zilizobaki ni kumalizia lami pamoja na kuhamisha mto ambao ulikuwa unakatisha katikati ya barabara ya kurukia ndege.
Aidha, alisema gharama za upanuzi wa uwanja huo kutoka urefu wa kilometa 3.3 hadi kufikia kilometa 3.8 katika njia ya kurukia ndege, jengo la mizigo na mnara, unagharimu Sh bilioni 105.
“Uwanja huu ukikamilika utasaidia kuimarisha uchumi wa mkoa wa Mwanza pamoja na usafirishaji kwa mikoa ya jirani pamoja na nchi za Kenya, Rwanda, Burundi na Uganda na kusafirisha mazao ya ziwani,” alisema.
Kaimu Meneja wa uwanja huo, David Matovolwa alisema kukamilika kwa uwanja huo kutasaidia ndege kubwa kutua pamoja na kuwekwa mafuta na kuruka kule ziendako bila wasiwasi.
Akizungumzia maendeleo ya uwanja huo, mkandarasi mshauri, Salem Munis alisema watajitahidi kuhakikisha uwanja huo unakamilika ndani ya kipindi cha miezi sita ijayo kama ilivyoagizwa na Profesa Mbarawa.
Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa alikagua daraja la waenda kwa miguu la Furahisha pamoja na barabara inayojengwa njia nne kutoka Furahisha hadi Uwanja wa Ndege wa Mwanza na kuridhishwa na maendeleo yake.
No comments:
Post a Comment