• Breaking News

    ..

    ..

    Friday, 16 September 2016

    WAZIRI MKUU MAJALIWA AHITIMISHA MKUTANO


    7
    Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akilihutubia Bunge kabla ya kutoa kauli ya kuliahirisha bunge hilo mpaka tarehe 1 Novemba 2016 ambapo mbali na mambo mengine amesema serikali itaendelea kutekeleza yale iliyoyaahidi na kuwashukuru wadau mbalimbali wanaoendelea kujitolea kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera, wakati wa kikao cha nane cha Bunge la kumi na moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
    Na Beatrice Lyimo na Eleuteri Mangi-MAELEZO, Dodoma
    Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amehitimisha Mkutano wa Nne wa Bunge la Kumi na Mbili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Mjini Dodoma.
    Akihitimisha Bunge, Waziri Mkuu ameainisha mambo mbalimbali ambayo yamefanyika wakati wa Mkutano huo ikiwa ni pamoja na mijadala mbalimbali inayohusu miswada ya sheria iliyosomwa kwa mara ya kwanza, mara pili na kwa mara ya tatu.
    Waziri Mkuu amesema kuwa mijadala ya mkutano huo ilikuwa ya uwazi na hoja zilizotolewa zililenga katika kuleta maendeleo nchini.
    “Nawapongeza sana wabunge wote kutokana na michango yenu mizuri na yenye tija hatua ambayo ilibidi mara kadhaa vikao vyetu kuendelea hadi usiku ikiwa ni nje ya muda wa kanuni za Bunge” amesisitiza Waziri Mkuu.
    Katika kuhitimisha mkutano huo, Waziri Mkuu amebainisha baadhi ya matukio mbalimbali yaliyotokea nchini ikiwemo janga la tetemeko la ardhi, shughuli za bunge, mwenendo na mwelekeo wa hali ya uchumi, mwenendo wa ukusanyaji mapato ya Serikali, mpango wa Serikali kuhamia Dodoma, hali ya upatikanaji wa chakula nchini, maboresho katika tasnia ya Ushirika, Sekta ya elimu, suala la uhakiki wa vyeti kwa watumishi, kuimarisha usafiri wa anga, hali ya amani na utulivu nchini pamoja na suala la michezo nchini.
    Akizungumzia kuhusu janga la tetemeko la ardhi lililotokea mikoa ya Kanda ya Ziwa, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wananchi, Sekta binafsi na Jumuiya za Kimataifa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kusaidia waathirika wa tetemeko hilo.
    “Serikali inaendelea kukusanya michango kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali, waliotayari kuchangia wanaweza kutumia akaunti ya maafa iliyofunguliwa benki ya CRDB yenye namba 0152225617300 kwa jina la Kamati ya Maafa Kagera na kwa njia ya simu michango hiyo inaweza kutumwa pia kupitia M-pesa 0768-196669, Airtel Money 0682-950009 na Tigo pesa 0718-069616” amesisitiza Waziri Mkuu.
    Kwa upande wa mwenendo na mwelekeo wa hali ya uchumi nchini, Waziri Mkuu amesema kuwa kwa ujumla hali ya uchumi nchini inaridhisha na inaendelea kuimarika.
    Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) hali ya uchumi umeimarika ambapo pato la Taifa lilikua asilimia 5.5 ikilinganishwa na asilimia 5.7 kwa mwaka 2015, ukuaji huo unatoka na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme, huduma za mawasiliano, utangazaji na huduma za intaneti na kuongezeka kwa uchimbaji wa madini.
    Katika suala la ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa mwezi Julai na Agosti, Waziri Mkuu amesema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi hicho mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yalikuwa shilingi Trilioni 2.168 ikilinganishwa na makadirio ya kukusanya shilingi trilioni 2.113 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 103 ya lengo la Serikali.
    Waziri Mkuu amesema kuwa, katika mpango wa Serikali kuhamia Dodoma ni dhamira ya Serikali ya Awamu ya tano ya kukamilisha mchakato na ahadi ya Serikali ya kuhamia katika Mji wa Makao Makuu Dodoma ambapo utekelezaji wake utakuwa wa awamu sita.
    Vilevile katika sekta ya Kilimo, Waziri Mkuu amesema kuwa hali uzalishaji na upatikanaji wa chakula nchini umefika tani 16,172,841, ambapo Serikali imetoa ruzuku za pembejeo za kilimo kwa ajili ya mazao ya chakula hususani mahindi, mpunga na mtama, kwa upande wa mazao ya biashara ruzuku hiyo hutolewa katoka mazao ya korosho, pamba, chai, kahawa na alizeti.
    Pia Serikali itafanya marekebisho ndani ya tume ya maendeleo ya Ushirika na kuchukua hatua za kinidhamu kwa watakao bainika na ubadhirifu wa mali za ushirika.
    Katika Sekta ya Elimu, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Serikali imeamua walimu wapya watakaoajiriwa wapangiwe vituo vya kazi moja kwa moja na kwa kuzingatia maeneo yenye upungufu wa walimu.
    Kuhusu uhakiki wa vyeti vya watumishi, Waziri Mkuu amesema kuwa, Serikali inaendelea na zoezi la uhakiki wa vyeti vya watumishi na kuwaagiza wagurugenzi wa halmashauri kuandaa vituo maalum ambavyo vipo jirani na vituo vya kazi ili kuwapunguzia watumishi gharama na adha wakati wa zoezi hilo.
    Katika kuboresha usafiri wa anga nchini, Waziri Mkuu amesema kuwa  Serikali imenunua ndege mbili aina ya Dash 8-Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja zitakazotumika kutoa huduma za usafiri wa anga kwa soko la ndani na chi jirani.
    Hata hivyo Waziri Mkuu amesema kuwa vyombo vya usalama na ulinzi nchini vimeendelea kulinda na kudumisha amani na utulivu nchini kwa manufaa ya ustawi wa nchi ili kufanikisha lengo la kukuza uchumi na kuondoa umaskini.
    Aidha, Waziri Mkuu ameipongeza Timu ya Taifa ya Vijana Serengeti Boys kwa kuiwakilisha vyema Tanzania katika mashindano ya Kimataifa.
    Mbali na hayo Waziri Mkuu Majaliwa amepokea michango mbalimbali iliyotolewa na Kampuni ya Caspian shilingi milioni 100, Ofisi ya Taifa ya Takwimu shilinhi milioni 1.6 na kampuni ya Bordar Ltd shilingi milioni 20 kwa ajili ya waadhirika wa tetemeko lililotokea mwishoni mwa wiki iliyopita katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa.

    No comments:

    Post a Comment

    HABARI

    HABARI

    MICHEZO

    LOGO

    LOGO

    MAOJIANO

    BURUDANI