• Breaking News

    ..

    ..

    Friday, 23 September 2016

    Waziri Nape kuitajirisha



    WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ametoa ahadi ya Sh milioni moja kwa kila bao watakalofunga wachezaji wa timu ya soka ya taifa ya bara ya wanawake Kilimanjaro Queens itakapocheza na wabunge wanawake Novemba mwaka huu.
    Nape aliyasema hayo kwenye chakula cha jioni na wachezaji wa timu hiyo walipowasili kutoka Uganda walipotwaa taji la Kombe la Chalenji kwa wanawake.
    “Nimetoa ahadi kwa wenzenu wa Serengeti Boys (Timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17) kwamba wakifunga bao nitawapa Sh milioni 1, sasa leo (juzi) naahidi hapa kwamba nitawaita Dodoma (bungeni) na mtacheza mechi na wabunge wanawake, kila bao nitatoa Sh milioni 1, sasa kama mtafunga 20 haya,” alisema.
    Akizungumzia ubingwa huo ambao Kili Queens imeutwaa kwa mara ya kwanza, Nape alisema ni rekodi ambayo haitavunjwa.
    “Yaani mashindano haya yamefanyika kwa mara ya kwanza na nyie (Kilimanjaro Queens) mmekuwa mabingwa wa kwanza hii ni rekodi ambayo haitavunjwa, kwani hakutakuwa na mabingwa wa kwanza wengine,” alisema.
    Alisema Kilimanjaro Queens imeiletea heshima serikali yake na kwamba anaahidi kuwatafutia wafadhili.
    “Mimi naingia mwenyewe kuwatafuta wafadhili wa timu hii, mmefanya vizuri nawaahidi hamtakosa… mfadhili,” alisema.
    Kisha akatania: “Kama kuna mfanyabiashara anataka tufumbe jicho moja kwenye kodi basi afadhili timu hii”.
    Aidha Nape alisema timu hiyo imewafurahisha wadau wa michezo mpaka Rais John Magufuli ametuma salamu za pongezi kwa mara ya kwanza kwenye michezo.
    “Mimi mwenyewe nimeshangaa, kuna wakati nilimwambia mzee Samatta (Mbwana anayecheza soka ya kulipwa Genk ya Ubelgiji) amefanya vizuri basi tumwite kidogo Ikulu, akasema subiri… sasa hili la Kili naona limemfurahisha zaidi,” alisema.
    Kilimanjaro Queens ilitwaa ubingwa kwa kuifunga Kenya mabao 2-1 katika michuano hiyo inayosimamiwa na Baraza la Vyama vya soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ambayo imefanyika kwa mara ya kwanza.

    No comments:

    Post a Comment

    HABARI

    HABARI

    MICHEZO

    LOGO

    LOGO

    MAOJIANO

    BURUDANI