MAHAKAMA ya Rufani imemhukumu kunyongwa hadi kufa aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni (OC-CID), Mrakibu wa Polisi (SP) Christopher Bageni, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la mauaji ya watu watatu.
Aidha imemuachia huru aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam (RCO) Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe na maofisa wengine wawili wa Polisi, Ahmed Makelle na Rajabu Bakari, baada ya kuwaona hawana hatia.
Baada ya kutolewa kwa adhabu hiyo, huzuni, simanzi na vilio vilitanda katika viwanja vya mahakama hiyo. Bageni aliondolewa kwenye viwanja vya mahakama hiyo saa tisa alasiri akiwa chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Magereza kwa kutumia gari lenye namba za usajili T 717 DVB.
Hukumu hiyo ilisomwa jana na Msajili wa Mahakama hiyo, John Kayoza kwa niaba ya Jopo la Majaji watatu waliosikiliza rufaa hiyo ambao ni Bernard Luanda, ambaye ndiye kiongozi wa jopo, na wengine ni Sauda Mjasiri na Semistocles Kaijage.
Akisoma hukumu hiyo, Kahyoza alisema baada ya Mahakama kufuatilia ushahidi uliokuwa umetolewa na upande wa Jamhuri, walibaini kuwa, wakati mauaji hayo yakitokea Bageni ndiye aliyekuwa kiongozi wa jopo la askari waliotekeleza mauaji hayo.
Alisema ahakama hiyo, imebaini kuwa Bageni alikuwa na uwezo wa kuamuru mauaji hayo yasifanywe na askari hao waliokuwa chini yake, badala yake alishindwa kufanya hivyo.
Kahyoza alisema baada ya kupitia rufaa hiyo, wanakubaliana na hoja za rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na kumtia hatia Bageni kati ya warufani wanne.
Akisoma adhabu hiyo, Kahyoza alisema, Bageni anahukumiwa adhabu ya kifo kwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kosa la mauaji katika mashitaka manne. Katika rufaa hiyo, DPP alipinga hukumu ya Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, iliyowaachia washitakiwa hao katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu.
Vilio mahakamani Baada ya hukumu hiyo kutolewa, ndugu waliofika mahakamani hapo akiwemo mke wa Bageni, waliangua kilio na wengine wakiwa na huzuni na kuwapa pole ndugu wa Bageni. Zombe alionekana kuwa na furaha, huku baadhi ya ndugu wakiwa karibu naye na kumfariji.
Adhabu hiyo imekuwa ya kwanza kutolewa dhidi ya askari wa Jeshi la Polisi hapa nchini. Kwa upande wa ndugu wa watu waliouawa, Diwani wa Kata ya Nawenge, Ulanga Mashariki, Protas Lungumbi (CCM), alisema wameridhika na hukumu iliyotolewa kwa kuwa haki imetendeka lakini walitaka Zombe awajibishwe hata kwa kifungo cha miaka michache jela.
Alisema kaka yake (ambaye aliuawa) amemuachia watoto wadogo ambao anawasomesha na wengine wamefika elimu ya Chuo Kikuu. Maelezo ya rufani Katika rufaa hiyo, DPP alidai kuwa Jaji Salum Massati alikosea kuwaachia huru washitakiwa hao kwa sababu kulikuwa na ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani wote.
Mbali na Zombe, wajibu rufaa wengine walikuwa ASP Christopher Bageni, ASP Ahmed Makelle, Konstebo Jane Andrew, Konstebo Emanuel Mabula, Konstebo Michael Shonza, Koplo Abeneth Salo, Koplo Rajabu Bakari na Koplo Festus Gwabisabi.
Katika kesi ya msingi inadaiwa Januari 14, 2006, katika msitu wa Pande uliopo Mbezi Luis, Dar es Salaam Zombe na wenzake waliwaua kwa makusudi wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Morogoro, Mathias Lunkombe, Sabinus Chigumbi na ndugu yake Ephrahim Chigumbi, pamoja na dereva teksi Juma Ndugu.
Baada ya kusikiliza kesi hiyo, Agosti 17, 2009, Jaji Massati aliwaachia huru washitakiwa kwa kuwa upande wa Jamhuri ulishindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao bila kuacha shaka na mahakama ikiwaona hawana hatia kwa makosa yaliyokuwa yanawakabili.
Oktoba 6, 2009, DPP alikata rufaa Mahakama ya Rufani, akipinga hukumu hiyo kwa madai kuwa Jaji Massati alikosea kuwaachia huru washtakiwa hao, pia kulikuwa na ushahidi wa dhahiri na wa kimazingira unaotosha kuwatia hatiani washtakiwa wote.
No comments:
Post a Comment