WABUNGE na wananchi wametakiwa kuheshimu sheria na kutahadharishwa juu ya ukiukwaji wa mikataba ya madini iliyoingiwa kati ya serikali na kampuni za uchimbaji madini hapa nchini ili kuepuka migogoro.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ametoa tahadhari hiyo bungeni mjini Dodoma. Amesema serikali imesaini mikataba ya madini na ipo Sheria ya Madini ya mwaka 2010 hivyo inatakiwa kuheshimiwa ili kuepuka serikali kushtakiwa.
Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Geita, Musukuma Kasheku(CCM) aliyetaka kufahamu serikali itawarudishia lini wananchi maeneo ya Samina na Nyamatagata yaliyoombwa na wananchi kupitia vikao vyote hadi mikoani na lini Shirika la Madini (Stamico) Nyarugusu litafanya kuwa la wachimbaji wadogo.
Waziri Muhongo akijibu swali hilo, alikiri kuwepo mgogoro mkubwa katika eneo hilo na kesi iko mahakamani, hivyo wananchi wawe watulivu kwani eneo hilo hawezi kugawiwa mpaka kesi iishe. Kwa mujibu wa Muhongo, leseni katika eneo hilo inamilikiwa na Stamico na kampuni ya Watanzania na raia wa Canada.
"Tumesaini mikataba, tukicheza tutashtakiwa. Labda wabunge wakubaliane nami serikali ikishtakiwa muwe tayari kulipa fidia au mwenendo wa kesi," alisema.
Alisema lazima watanzania wapewe elimu juu ya kuheshimu mikataba hiyo ya uchimbaji madini ili kuepuka kuingia migogoro na kampuni kubwa za uchimbaji madini hapa nchini.
Kuhusu ruzuku kwa wachimbaji wadogo, Muhongo alisema walibaini katika awamu ya kwanza na ya pili ruzuku za vifaa iliyokuwa imetolewa kwa wachimbaji hao havikufika katika migodi.
"Tunafanya tathmini sasa kabla ya kutoa ruzuku ya awamu ya tatu, maana nilipita kukagua nikakuta vifaa havijafikishwa katika maeneo husika, kwa hiyo kuna ukikwaji wa matumizi ya ruzuku hiyo," alisema.
Awali akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Medard Kalemani alisema eneo la Samina na Nyamatagata yako ndani ya leseni ya uchimbaji mkubwa wa madini ya dhahabu ya Kampuni ya Geita Gold Mining Limited, lakini serikali inaendelea na mazungumzo na mgodi huo ili kampuni iweze kuachia baadhi maeneo isiyohitajika kwa lengo la kuwamilikisha wachimbaji wadogo.
Alisema eneo la Stamico la Nyarugusu ambalo lipo kitongoji cha Buziba lina leseni ya utafiti inaomilikiwa kwa ubia asilimia 45 na 55 kati ya Stamico na Kampuni ya Tanzam 2000 na itaisha muda wake Julai 11, 2018.
No comments:
Post a Comment